ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ametoa kauli nzito, baada ya kusema viongozi wa vyama vya siasa wanaopekua mawasiliano ya raia ni hatari kwa nchi na kwamba wakishika dola, raia wao hawatapona.
Kauli ya Zitto imekuja siku moja tu baada ya
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbrod Slaa, kuutangazia umma kuwa
wamenasa mawasiliano ya siri yanayodaiwa kufanywa na Zitto. Zitto
aliliambia MTANZANIA jana kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu kwamba sheria
za nchi zinazuia mtu kupekuliwa mawasiliano yake.
“Sheria za nchi zinazuia mtu kupekuliwa pekuliwa mawasiliano, haki ya faragha ni haki yangu ya msingi.
“Kama
viongozi wa chama cha siasa cha upinzani wanafanya kazi ya kupekua
mawasiliano ya raia na kujiona wanafanya sahihi, watu hao ni hatari kwa
nchi, maana wakishika dola raia hawatapona. Mimi siwajali watu hawa,
nawadharau,” alisema Zitto.
Akizungumzia uamuzi wa kuvuliwa
uanachama kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson
Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo, Zitto alisema chama
kimefanya uamuzi wake.
“Chama kimefanya uamuzi wake na ni wajibu
wao akina Kitila na Mwigamba kuona kama wanapaswa kukata rufaa au
hapana,” aliongeza Zitto.
Aidha amesikitishwa na kauli ya Dk.
Slaa kuzuia wanachama wake kushiriki mikutano yake ya kisiasa, kwani
kufanya hivyo ni kukosa busara.
“Kwangu mimi, uamuzi wa Katibu
Mkuu kuzuia viongozi na wanachama kushiriki mikutano yangu nadhani ni
kukosa busara na hekima, suala langu bado liko mahakamani, likitoka
litarudi kwenye chama.
“Nasisitiza, kutangaza namna hii si sawa kabisa kwa mujibu wa misingi yote ya demokrasia,” alisema Zitto.
>>Mtanzania.
>>Mtanzania.