Siri ya mafanikio St Francis

Mbeya/Dar. Mkuu wa Shule ya Sekondari St Francis ya mkaoni Mbeya iliyoshika nafasi ya kwanza kitaifa katika Matokeo ya Kidato cha Nne yaliyotangazwa jana, Sista Flossy Sequira amesema kuwa alikuwa na uhakika kwamba shule yake ingefanya vizuri kwenye mtihani huo, huku akitaja siri ya mafanikio.
“Tumefurahishwa na matokeo licha ya kuwa tulikuwa tunafahamu fika kuwa tutafanya vizuri kwa kuwa huo ndiyo utamaduni wetu, tutahakikisha tunaendelea kushika nafasi hiyo kila mwaka,” alisema Sista Sequira.
Alipotakiwa kueleza siri ya matokeo hayo kwa shule yake kila mwaka, mkuu huyo wa shule alisema: “Siri kubwa ya mafanikio hayo ni kumtanguliza Mungu kila siku na ushirikiano wa hali ya juu uliopo kati ya walimu, wanafunzi na uongozi wa shule.”
Aliongeza kuwa umakini walionao wanafunzi wa shule hiyo ni sababu nyingine ambayo huwarahisishia walimu wakati wa kufundisha, hata wanapowatolea majaribio ya mara kwa mara.
Naye Mkuu wa Shule ya Wasichana ya Canossa ya Dar es Salaam, iliyoshika nafasi ya tano Yvonne D’souza, alisema amefurahi kuwa mwanafunzi aliyeshika nafasi ya tatu katika kumi bora ametoka shuleni hapo, lakini alitarajia wangefaulu wanafunzi zaidi ya watatu katika kundi hilo.
“Kufaulu ni kawaida yetu, sisi tunafuata viwango vya elimu vinavyotakiwa. Mwaka huu nimefurahi kwa sababu wasichana ndiyo waliofaulu zaidi, ninataka wapande, wawe juu, huu ni wakati wao,” alisema D’souza.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Wasichana ya Marian, Flora Mapunda, ambaye shule yake imetoa wanafunzi wanne bora ikishika nafasi ya sita, alisema matokeo hayo hayakumridhisha sana kwani alitegemea wanafunzi wengi wangefaulu zaidi.
Katika matokeo hayo yaliyotolewa na Baraza la Mtihani la Tanzania na kutangazwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa baraza hilo Dk Charles Msonde, Sekondari ya St Francis imekuwa ya kwanza, ikifuatiwa na Marian Boys ya mkoani Pwani, huku Feza Girls ya jijini Dar es Salaam ikiwa nafasi ya tatu.
Katika shule hizo kumi bora, Sekondari ya Precious Blood ya Arusha imekuwa ya nne, Cannosa ya Dar es Salaam imekuwa ya tano, Marian Girls ya Pwani nafasi ya sita, Anwarite Girls ya Kilimanjaro ipo nafasi ya saba.