CHADEMA yakituhumu chama cha CUF kwa kuandaa vijana wenye panga na marungu ili wakamuunge mkono Zitto Kabwe...CUF yakanusha




MGOGORO unaoendelea Chadema umefikia hatua ya kuanza kutafuta mchawi ndani na nje ya chama hicho, ambapo sasa kimeishika CUF na Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono kwa madai ya kumwunga mkono aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Kabwe Zitto
.
 
Juzi wakati akitangaza kuwavua uanachama aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu wa Chama hicho, Dk Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, John Mnyika alisema wapo katika vita dhidi ya maadui wa nje na ndani ya chama na watapambana mpaka mwisho.
 
Jana taarifa kutoka ndani ya Chadema zilidai kuwa Mwenyekiti wa Chadema Temeke, Joseph Patrick, alishirikiana na Mkurugenzi wa Sera na Haki za Binadamu wa CUF, Abdul Kambaya, kutafuta vijana wa kwenda kumuunga mkono Zitto Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakati wakisubiri hukumu kuhusu uanachama wake.
 
Hata hivyo, Jaji John Utamwa anayesikiliza kesi hiyo, aliahirisha kusoma uamuzi huo hadi leo saa 8 mchana, kwa kuwa bado hajakamilisha.
 
Pia taarifa zilisambaa kuwa kiongozi wa Chadema ambaye ni Mwanasheria anayeunga mkono upande wa Mwenyekiti Freeman Mbowe, alimtuhumu Mkono kwa kumpa Zitto magari mawili ili ahujumu chama hicho katika uchaguzi mkuu uliopita.
 
Tuhuma CUF
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, akina Kambaya wanadaiwa kupanga watu walioitwa wahuni mahakamani jana kwa kuwapa fulana za Kampeni ya Kuhamasisha Mabadiliko (M4C) na Sh 20,000.Watu hao wanadaiwa kuvuta bangi hadharani na kupewa visu na mapanga ili kumlinda na kumwunga mkono Zitto.
 
“Hii yote ni kazi ya uratibu wa kambi ya Zitto. Lengo ni kutaka kumwaga damu za watu ionekane Chadema wamekatana mapanga. “Hiyo ni mbali ya wahuni walionunuliwa kubeba mabango na kuimba nyimbo mahakamani kama ilivyokuwa Kigoma,” ilieleza taarifa hiyo kutoka chanzo kinachoaminika na kinachounga mkono uongozi wa Mbowe.
 
Vurugu mahakamani
Taarifa hiyo ilitolewa muda mfupi, baada ya kuibuka kwa mvutano nje ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kati ya wana Chadema wanaomwunga mkono Zitto na akina Mbowe.
 
Wanachama hao wa Chadema walifurika mahakamani katika kile kilichoonekana ni kuitika mwito wa Mnyika, alioutoa juzi kuwataka wajitokeze jana mahakamani kuonesha mshikamano na nguvu ya umma.
 
Tofauti na matarajio ya Mnyika, wafuasi wa Chadema walipofika mahakamani waligawanyika kambi mbili; ya Zitto-ambao taarifa hiyo ilidai wameandaliwa na CUF - na ya Mbowe, wakioneshana nguvu ya umma wao kwa wao.
 
Askari Polisi waliokuwa wameimarisha ulinzi, walizunguka eneo la Mahakama wakiwa na mbwa, mabomu ya kutoa machozi na gari la maji ya kuwasha na kila aliyeingia alikaguliwa na kujiandikisha.
 
Wafuasi hao walikataliwa kuingia eneo la Mahakama na kuamriwa wakae kando ya barabara, lakini baadaye baadhi waliruhusiwa baada ya kukaguliwa na kutambuliwa na viongozi wao wa matawi.
 
Waliobaki nje ya Mahakama walichora mstari katikati na kuamuru wafuasi wa Mbowe wasifike upande wa wale wa Zitto. Hata hivyo mfuasi mmoja alivuka kwenda upande wa Zitto, wakampiga na kumrudisha upande wake, huku wakiendelea kuimba wakiwa na mabango ya kumsifu Zitto.
 
CUF yajibu  mapigo:
Taarifa hizo zilifika CUF, ambapo walijibu haraka kwamba chama hicho hakijapanga wala kutuma makundi ya vijana kwenda kumshabikia Zitto kama inavyodaiwa na Chadema.
 
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro, alisema kama kuna wanachama wa chama chake wameonekana mahakamani wakati wa kesi hiyo watakuwa wamekwenda kwa utashi na matakwa yao na si kutumwa na chama.
 
Mtatiro alitoa taarifa kwa maelezo kuwa baadhi ya waandishi wengi wa habari walimpigia simu athibitishe ikiwa CUF iliandaa makundi ya wanachama wakamshabikie Zitto mahakamani jana na taarifa ya namna hiyo pia ilikuwa kwenye mitandao ya kijamii.
 
“Pia viongozi kadhaa wa Chadema wamenipigia kunijulisha kuwa intelijensia yao imegundua kuwa vijana wa CUF wamepenyezwa na wamevishwa fulana za M4C na kupewa mapanga. “Sisi chama Taifa hatujawahi kukutana, kupanga wala kutuma vijana wa CUF wakasimamie upande wowote katika mgogoro huu. Wakati wa fukuto la Hamad Rashid Mohamed na CUF watu wengi raia walifika mahakamani, sisi hatukuhoji na kutafuta vyama vyao, tuliamini ni Watanzania,” ilisema taarifa ya CUF.
 
Ushauri Chadema
Naibu Katibu Mkuu huyo alitoa ushauri, kwamba panapokuwa na kesi inayovuta hisia za watu, vyama vya siasa au wahusika wasihoji watu hao wanatoka makundi gani, kwani haki zinawapa uhuru wanaotaka kwenda kusikiliza kesi hiyo kufanya hivyo bila kikwazo.
 
Alisema ni vigumu kwa CUF kukataza wanachama kuhudhuria kesi ya Babu Seya, ya Shekhe Ponda, ya Zitto au ya Samaki wa ‘Magufuli’.
 
“Unapokuwa na chama chenye maelfu ya wafuasi, si rahisi kujua mfuasi yupi yuko wapi kwa wakati gani na anafanya nini na ametumwa na nani.”
 
Alisema kwa ajili ya kujenga mshikamano wa vyama vya upinzani, CUF inachunguza taarifa hizo ili kubaini kama kweli kulikuwa na wanachama wake mahakamani na wakiwabaini watawahoji na kujua nani aliyewatuma na wataona hatua za kuchukua.
 
“Ikumbukwe, kuwa Mwenyekiti wa Chama chetu, Profesa Ibrahim Lipumba wakati akisoma maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa Desemba mwaka jana, alieleza kuwa Baraza Kuu la CUF linaomba Chadema wamalize mgogoro wao haraka, ili tuwekeze nguvu za upinzani katika kuunganisha umma kutafuta Katiba ya Watanzania kwenye Bunge la Katiba, Msimamo wa CUF ni kutokuwa na upande katika mgogoro huu,” alisema Mtatiro.
 
Alisema CUF itaendelea kuheshimu Chadema kama taasisi inayojitegemea. “Hatukuwahi kuingilia, kushabikia wala kupinga masuala na uamuzi wa ndani ya Chadema, tukiona pana jambo linatugusa mara zote huwa tunatoa ushauri wetu tu na si kuingilia masuala ya ndani ya vyama vingine.”