MKE wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria, amesikitishwa na jinsi baadhi ya watu wanavyomkosoa mwasisi huyo kwa kuwa enzi za uhai wake alifanya kazi kwa bidii katika kulitumikia taifa kiasi cha wakati mwingine kuisahau familia kwa muda.
Akiongea na waandishi nyumbani kwake Msasani, jana, Mama Maria alisema kwa uchungu kuwa mumewe ambaye alifariki miaka 15 iliyopita, amemtokea ndotoni na kumtaka akalitahadharishe taifa na mwenendo wake.
“Kitendo cha nchi kukumbwa na mashetani wanaovuruga amani na kutukana waasisi kimemfanya Mwalimu Nyerere kunitokea na kunitaka kuliambia taifa kusali na kuomba sana kwani nchi inaelekea katika vita” Alisema jana huku akionesha hisia kali.
Pia, alisema mambo yanayoendelea nchini kwa sasa ni matokeo ya tamaa na kupungua kwa upendo miongoni mwa jamii jambo linalohatarisha usalama na amani ya nchi.
Mama Maria
alisema ukosoaji wa viongozi waasisi ni tatizo la dunia nzima ambalo
limekuwa jinamizi kama ilivyotokea kwenye nchini mbalimbali ikiwemo
Misri na Libya, hivyo ili Tanzania iweze kuepukana nalo ni wajibu wa
kila mtu kuombea taifa kwa kufikiria tulikotoka na tulipo.
Alisema ni wazi
kuwa Mwalimu Nyerere alifanya kazi kwa bidii hata kuisahau familia muda
mwingine, kwa sababu aliwapenda Watanzania pasipo ubaguzi wowote na
kama alikosea mahali ilitokea kwa kuwa na yeye ni binadamu. Hivyo
haipaswi watu kumsema tofauti kama wanavyomsema sasa.