Aliyekuwa mbunge wa Songea mjini, Abdulrabi Ali Yusuph(66) akizungumzia maisha yake baada ya kufungwa
Aliyekuwa Mbunge wa Songea mjini kuanzia Oktoba 1985 hadi Aprili 1988 alipofungwa jela miaka 11, Abdulrabi Ali Yusuph (66), amesema tangu atoke gerezani hadi sasa anaomba aonane na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi ama Rais Benjamin Mkapa na hata Rais Jakaya Kikwete lakini hajafanikiwa hadi leo.
Amesema
aliomba nafasi ya kumwona Rais Mwinyi akiwa madarakani ili amweleze ya
moyoni, lakini hakufanikiwa na aliendelea kuomba amwone Rais Mkapa
hakufanikiwa na sasa anaomba amwone Rais Kikwete bado hajajaaliwa.
Alisema
hayo katika mahojiano maalumu yaliyofanyika nyumbani kwake Mtaa wa
Mfaranyaki mjini Songea ambako anaishi akiwa kwenye nyumba chakavu ya
urithi na wake zake wawili pamoja na watoto kadhaa.
Mahojiano ya mwandishi na mbunge huyo yalianza hivi.
Mwandishi:
Mheshimiwa habari za siku nyingi. Nimefika hapa kwa niaba ya jarida la
Ndani ya Habari linalochapishwa na gazeti la Mwananchi, lengo hasa ni
kukujulia hali. Watu wangependa kujua unaendeleaje hasa baada ya
kifungo chako. Ningependa kupata maelezo yako juu ya masuala ya maisha
ya gerezani na ya sasa ukiwa huru.
Mbunge. Kwanza kabla ya yote. Wewe upo hapa ili uuze gazeti na upate fedha. Je, mimi unanieleza vipi kuhusu mapato hayo.
Mwandishi:
Kazi ya mwandishi siyo biashara, bali ni ya kijamii. Kazi ya mwandishi
ni kuelimisha, kufundisha, kuibua kero na kutaarifu jamii. Kazi ya
mwandishi inaweza kukusaidia ama kukuharibia kwa kuibua mambo ambayo
unaweza kufanya kwa kuvunja sheria na kuitisha jamii.
Mbunge: Kwa maneno yako haya ni kwamba mimi sina lolote la kufaidika leo?
Mwandishi: Ni
kweli sikuja hapa kibiashara bali kukusalimu na kupata hisia zako ama
kauli yako baada ya kufungwa jela kwa miaka 11 ukiwa mbunge na sasa
upo nje, hivyo tunapenda kujua uliishi vipi jela na jamii inakuonaje
baada ya kutoka?
Mbunge:Basi
kwa kuwa umefika hapa, nitasema machache, lakini kama utakuja baada ya
kujipanga, nitaeleza mengi mno. Mimi ninazo kero na mambo mengi baada
ya kuishi gerezani na kwa kweli nina masikitiko mengi ambayo
yananisononesha sana.
Mwandishi:Nashukuru Mheshimiwa, naomba udokeze hisia zako walau kidogo.
Mbunge:
Kwanza ninayo masikitiko mpaka leo kwa viongozi wakuu wa taifa hili.
Nasikitika mpaka leo kwa kunyimwa nafasi ya kuonana na walau mmoja
kuanzia Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, awamu ya tatu,
Benjamin Mkapa na hata awamu ya nne Jakaya KIKWETE
Mimi
ninayo mambo mengi sana kwa viongozi wetu, Serikali na hata kwa taifa,
lakini nasikitika kuona waliokuwa viongozi wenzangu wamenitenga kana
kwamba mimi ni shetani’’ anasema.
Mimi
nilibambikiwa meno ya tembo na hatimaye nilifungwa jela, nilichojifunza
cha kwanza ni kwamba jamii ina tabia ya kuwanyanyapaa waliowahi
kufungwa jambo ambalo hata viongozi wa taifa nao wanatekeleza kwa
vitendo juu yangu. Wapo viongozi wenzangu ambao wakati ule tulicheka
pamoja, tulikula pamoja na kucheza pamoja, lakini baada ya mimi kwenda
jela hawaonekani.
Kufungwa kwangu kulipangwa
Mwandishi:Unasikitika kwa kufungwa kwako ama kunyanyapaliwa?
Mwandishi:Unasikitika kwa kufungwa kwako ama kunyanyapaliwa?
Mbunge:Mimi
baada ya kufika gerezani nilijiuliza swali la kwanini nimefungwa?
Maana ukweli ni kwamba meno ya tembo siyo yangu. Baadaye nilipata jibu
kwamba nilifungwa ili nikaone mambo maalumu magerezani. Mambo
niliyoyashuhudia yanatisha. Lakini la kwanza ni kwamba siyo wote
wanaofungwa wanatenda makosa waliyoshtakiwa nayo. Pili niligundua
kwamba askari magereza si wabaya wakiwa kazini, bali wabaya ni
waliokupeleka kwao.
Pia
nilijifunza kwamba askari magereza wanafanya kazi katika mazingira
magumu kiasi kwamba wanafika hatua ya kuomba msaada kwa wafungwa. Pia
niliona wazi kwamba wapo wafungwa wanaorudi gerezani kwa kupenda huku
wengine wakirudishwa gerezani kwa hila za udhalimu.
Nilishuhudia
kunyongwa kwa wafungwa 11 na nilishiriki kusafisha vitanzi vyao,
miongoni mwao, wapo walionyongwa huku wakikana kutenda makosa
waliyoshtakiwa nayo.
Mwandishi: Maisha yalikuwaje gerezani?
Mbunge:Baada
ya kuhukumiwa kufungwa nilitoka gereza la Songea kwenda gereza la
Lilungu Mtwara, baadaye nilipelekwa Ukonga Dar es Salaam na hatimaye
Gereza la Maweni Tanga. Cha kushangaza katika magereza yote mimi
nilikuwa mnyapala mkuu na pia imamu wa kuswalisha Waislam waliofungwa.
Aporwa mke baada ya kufungwa
Mwandishi:Ukiwa jela , je uliifikiriaje familia yako?
Mbunge:Kwa
kweli nasema wazi kwamba suala la kufungwa kwangu lilipangwa na watu
mbalimbali. Nasema hivi kwa sababu baada ya miezi mitano hivi ,
kiongozi wa dini ya Kilokole alinifuata nikiwa Gereza la Lulindi na
kuniambia kwamba mke wangu alimbadilisha dini na kuwa mlokole na
aliamua pia kumuoa.
Mwandishi: Kwa hali hiyo huna mke mpaka sasa?
Mbunge. Hapana, kwa sasa nina wake wawili na watoto, watoto, eeeh nina watoto kadhaa.
Mwandishi: Ulifungwa
miaka tisa nwaka 1988 , lakini ulikata rufaa ambayo ulishindwa na
hatimaye kufungwa miaka mitatu zaidi, lakini ulitoka kwa msamaha wa
Rais ikiwa imebaki miezi minne, je ulijisikiaje?
Mbunge:
Nakumbuka nilitolewa siku ya Ijumaa. Basi nikaanza kuifikiri sana siku
hiyo kuwa ina maana kubwa kwangu. Nasema hivyo kwa sababu nilizaliwa
Ijumaa, nilikamatwa kwa tuhuma za meno ya tembo siku ya Ijumaa,
nilihamishwa kutoka Songea kwenda Lulindi siku ya Ijumaa na hatimaye
kuachiwa siku ya Ijumaa. Jambo hili lilinipa wasiwasi na kujiuliza
mara kadhaa maana yake ninni. Lakini mama yangu mzazi aliyefariki mwaka
juzi nakumbuka alinisihi nimshukuru sana Mungu kwa siku yake ya Ijumaa
kuifanya kuwa ya matukio makuu.
Mwandishi:Ukiwa gerezani kuna mambo gani unaoyakumbuka zaidi.
Mbunge:
Kwa kweli nayakumbuka yaliyokuwa yakitokea nje ya gereza juu yangu. La
kwanza linalonisikitisha sana ni taarifa ya Kiongozi wa Bunge (anamtaja
jina) ambaye aliwahi kulitangazia Bunge na Taifa kwa ujumla kwamba
aliyekuwa mbunge na kufungwa jela Abdulrabi Ali Yusuph amefariki dunia.
Jambo
hili lilinisikitisha sana. Nilimwambia Marehemu Dk Laurence Gama akiwa
mbunge jambo hilo kwamba nilikerwa sana na alinihakikishia kulimaliza.
Jambo
la pili lililonishtua ni kauli ya Rais wa awamu ya pili Ali Hassan
Mwinyi alipotamka kwamba Serikali yake haina upendeleo katika masuala
ya dini akitoa mfano kwamba padri Erio aliyekamatwa kwa makosa ya
kuvunja sheria aliamwaachia, lakini ameamua Muislam mwenzake akitaja
jina langu aendelee kusota jela. Kauli ile ilinihuzunisha kwa vile
kwanza kosa lilikuwa la kubambikiwa na pili kiongozi mkuu anatangaza
kuniacha nisote jela.
Mwandishi: Pamoja na kwamba unasema jamii ina mwelekeo wa kuwanyanyapaa wanaofungwa, je wapiga kura wako nao walitekeleza hayo?
Mbunge:
Baada ya kutoka gerezani, wapo wana CCM waliofika na kunitaka niwe
kiongozi ngazi ya wilaya, kata na hata mtaa, lakini nilisita sana
ingawa baadaye nilikubali kuwa Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mfaranyaki
hadi mwaka jana. Kwa ujumla utendaji wa CCM kwa sasa umebadilika sana.
Hauna shukrani hata kwa waasisi wake. Mimi nina historia ndefu ya Chama
hiki. Baba yangu marehemu Abdulrabi Yusuph ndiye aliyekuwa Katibu wa
kwanza wa Chama cha TANU. Baba yangu ndiye aliyefanya kazi na Nyerere
kwa dhati.
Mwandishi: Viongozi wa Serikali wanaweza kukusahau, je wale wa CCM nao?
Mbunge: Nakueleza
baada ya kufungwa, wana CCM walinisahau kabisa , lakini siku moja dada
yangu alikwenda Uwanja wa Majimaji alipotembelea Rais wa awamu ya pili
Ali Hassan Mwinyi na kumwangukia miguuni.
Askari na vyombo vya usalama vilitaka kumfunga dada yangu,
lakini Rais aliagiza mwanamke huyo afike Ikulu Songea ambako alikwenda
na kuomba Serikali isaidie kuwasomesha watoto wangu wawili ambao
alikuwa akiishi nao mimi nikiwa jela.
Basi
nashukuru Mwinyi aliagiza CCM iwasomeshe watoto wawili ambao kweli
walisomesha hadi kidato cha nne wakati mimi nikiwa jela.
MWANANCHI
MWANANCHI