IRAN WAPONGEZWA

     Raia wa Iran wakifurahia matokeo ya wajumbe walioshiriki mazungumzo yaliyofanikisha kupatikana kwa mkataba wa nyuklia kati ya Iran na mataifa sita makubwa duniani.Picha na AFP

Gumzo kuu linalotawala duniani kote hivi sasa ni hatua ya Iran na mataifa sita yenye nguvu za kijeshi na kiuchumi kufikia makubaliano mapema juzi kuhusu kudhibiti mpango wa Iran wa nyuklia, huku nchi hiyo ikifaidika kwa kupata unafuu wa vikwazo vilivyowekwa dhidi yake yapata miaka kumi iliyopita.
Makubaliano hayo ambayo hayakutarajiwa yameishangaza dunia. Hakuna aliyetarajia siyo tu kwamba Iran siku moja ingekubali kukaa meza moja na mataifa yenye urafiki mkubwa na hasimu wake Israel kuzungumzia udhibiti wa mpango huo, bali pia mataifa hayo ya Magharibi hayakutarajiwa kufanya mazungumzo na nchi hiyo wala kuipunguzia vikwazo vya kiuchumi kabla haijasitisha mpango huo, mbali na kulitambua rasmi ‘Taifa la Israel’
.
Itakumbukwa kwamba mchakato uliofanikisha makubaliano hayo ulianza kama mzaha miezi michache iliyopita kwa Rais mpya wa Iran, Hassan Rouhani kumpigia simu Rais Barrack Obama wa Marekani akitaka kurudishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili zenye uhasama mkubwa tangu wanamgambo wa Iran walipouteka Ubalozi wa Marekani nchini humo mwishoni mwa miaka ya 70. Huo ndio ulikuwa mwisho wa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili hadi leo.
Pamoja na baadhi ya Wamarekani kudai kwamba wito wa Rais Rouhani ulikuwa na ajenda ya siri, Rais Obama aliutafakari kwa hadhari kubwa na kuwataka wananchi wake kutoa nafasi kwa Iran kuthibitisha kama kweli ilikuwa na dhamira ya kutafuta amani. Baada ya kuridhika kwamba Iran ilikuwa na dhamira hiyo, aliyakutanisha mataifa sita yenye nguvu, yaani Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Russia, China na Uingereza na kuyashawishi kwa pamoja kufanya mazungumzo na Serikali ya Iran.
Mazungumzo yamekuwa yakifanyika mjini Geneva, Uswisi kwa wiki kadhaa na makubaliano ya mwisho yalifikiwa mwishoni mwa wiki baada ya siku nne za majadiliano. Makubaliano hayo yanachukuliwa kama hatua ya kwanza muhimu kuelekea kuondoa wasiwasi wa dunia kuhusu mpango huo wa nyuklia, lakini pia yanajumuisha udhibiti wa hali ya juu dhidi ya taifa hilo kujipatia silaha za nyuklia.
Kwa maana hiyo, Iran itasitisha urutubishaji wa kiwango cha juu cha madini ya urani na itafaidika kwa kuachiliwa kwa dola 4.2 bilioni zilizozuiliwa katika benki za kigeni, hivyo kuweza kuanza tena biashara ya madini ya thamani, bidhaa zitokanazo na mafuta pamoja na vipuri vya ndege.
Madini ya urani yaliyorutubishwa yanaweza kutumiwa kuendesha vinu vya nishati ya kinyuklia ambalo sisi tunadhani ndio hasa lengo la Iran, lakini pia yanaweza kutumiwa kutengeneza bomu la nyuklia iwapo yatarutubishwa zaidi.
Tunaipongeza Serikali ya Iran na wananchi wake kwa jumla kwa kuchagua amani badala ya vita katika Mashariki ya Kati ambapo umekuwapo uhasama mkubwa kati ya nchi nyingi za Kiarabu dhidi ya Israel, hasa kuhusu ‘Suala la Palestina’. Bila shaka kuzuka kwa vita katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta kungeiathiri dunia nzima kiuchumi na nchi maskini kama Tanzania ndizo zingeathirika zaidi.
Israel inamiliki silaha za nyuklia. Jambo la kushangaza ni kuwa, wakati dunia ikifurahia makubaliano hayo, Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu amesema makubaliano hayo ni ‘mabaya’. Msimamo huo unathibitisha madai kwamba kiongozi huyo amekuwa akifaidika kisiasa kutokana na mgogoro wa nchi yake na Iran.