Tundu Lissu: Wabunge wengi mbumbumbu





Tundu Lissu
MNADHIMU Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), amesema wabunge wengi wa Tanzania hawafahamu lugha ya Kiingereza, jambo linalowasababishia kupitisha miswada ya sheria mibovu. Lissu ambaye pia ni Mwanasheria wa Chadema, amesema tatizo la wabunge wengi kutojua Kiingereza ni janga linalotakiwa kutazamwa kwa kina, hasa kwenye Katiba Mpya.



Akizungumza katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV, Lissu alisema tatizo la wabunge kutofahamu lugha ya Kiingereza linaweza kuathiri baadhi ya mambo ya kisheria.

Alisema kumekuwapo na sheria nyingi ambazo zimekuwa zikipitishwa na wabunge bila kuzingatia umakini wa vifungu vya sheria yenyewe.


“Ikumbukwe kuwa zaidi ya asilimia 100 ya Watanzania wanazungumza Kiswahili, hivyo wanaozungumza lugha ya Kiingereza ni asilimia chache sana na hata akizungumza lazima atachanganya na Kiswahili.


“Hili ni tatizo ambalo limetokana na mfumo mbovu wa elimu nchini, hivyo ndio maana baadhi ya wabunge kule bungeni hawajui kabisa kuzungumza au kuandika Kiingereza, yaani muswada ukija wao wanalala wanashtuka na kupiga makofi basi muswada umepita.


“Ukishafika kwa wananchi na kuleta athari, ndipo wanapogutuka na kubaini wamepitisha muswada mbovu,” alisema Lissu.


Akizungumzia kauli hiyo ya Lissu, Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila alisema kuwa hawezi kuzungumzia kauli hiyo, kwani wabunge wote wamechaguliwa na wananchi jambo linalowapa mamlaka ya kuwawakilisha bila kujali kama wanajua ama hawajui.


Kwa upande mwingine, Lissu alizungumzia hali ya mivutano iliyopo ndani ya chama chao, ambapo alikiri mivutano hiyo kukiathiri chama.


Alisema kitendo cha baadhi ya viongozi wa chama hicho kutimuliwa kimezalisha pengo, ambapo pia kuna uwezekano mkubwa wa chama kupoteza baadhi ya wanachama ambao ni wafuasi wa viongozi waliotimuliwa.


Aidha alisema Kambi ya Upinzani Bungeni, imefanikiwa kupigania mchakato wa Katiba unaozingatia matakwa ya Watanzania, jambo ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.


“Tatizo limebaki kwa huu ufalme wa urais, kwa sababu rais ndiye anayewateua wajumbe, kila kitu kipo juu yake,” alisema.