
Rais Jakaya Kikwete
IKULU imetoa tamko zito dhidi taarifa za uzushi zinazoenezwa na Rwanda kuwa Rais Jakaya Kikwete alikutana kwa nyakati tofauti na viongozi wa makundi ya waasi yanayopingana na Serikali ya Rais Paul Kagame.
Taarifa iliyotolewa kwa pamoja Dar es Salaam jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, na ubalozi wa Tanzania mjini Kigali, ilisema Rais Kikwete amesema ameumizwa na uongo huo uliochapishwa na Gazeti la Serikali ya Rwanda la The News of Rwanda.
Mwishoni mwa wiki gazeti hilo lilichapisha taarifa iliyomtuhumu Rais Kikwete kuwa anasaidia kwa namna moja au nyingine kuwezesha vikao na makundi ya waasi wanaoipinga Serikali ya Kigali.
“Gazeti la The News of Rwanda, ambalo linajulikana kwa sifa mbaya na hatari ya kuandika propaganda chonganishi na za uongo, lilidai kukariri vyanzo vya habari ambavyo halivitaji.
“Linadai pamoja na mambo mengine kuwa waanzilishi wawili wa kundi la Rwanda National Congress (RNC), akiwamo Dk. Theogene Rudasingwa walikutana kwa siri mjini Dar es Salaam na makamanda waandamizi wa waasi wa Rwanda, The Democratic Forces for Liberation of Rwanda (FDLR).
“Rais Kikwete ameumizwa sana na uongo huu na ametoa ushauri wa kiungwana kwa wahariri wa chapisho hilo kuacha kutengeneza madai ya kutunga na yasiyo na chembe ya ukweli ambayo yanaweza kutengeneza uhasama, uadui na mkanganyiko baina ya watu wa nchi hizi rafiki na jirani.
“Wakati ikijulikana wazi kwamba Rais Kikwete na Rais Paul Kagame wa Rwanda walikubaliana mjini Kampala, Uganda kuendeleza uhusiano wa kirafiki baina ya nchi hizi, madai haya mapya yanachoweza kufanya ni kuchafua hewa na Rais Kikwete angependa kujua ajenda gani walizo nazo wahariri wa chapisho hilo?” iliuliza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo, ilisema Ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda hauwezi kuchukulia kwa urahisi tuhuma hizo kwa vile zinaonekana wazi zina lengo fulani.
Kaimu Balozi wa Tanzania nchini humo, Francis Mwaipaja katika taarifa yake alisema gazeti hilo limekusudia kuchafua sifa ya Tanzania.
“Kwa kweli, ripoti hizi hazina ukweli wowote zaidi ya kuwa ‘lundo’ la uongo hatari uliotengenezwa na wahariri wa chombo hicho kwa lengo la kumshambulia binafsi Rais wa nchi rafiki na jirani na kutaka kutengeneza taswira kwamba Tanzania inashirikiana na maadui na makundi yanayoipinga Serikali ya Rwanda.
Ubalozi wa Tanzania nchini Rwanda katika ufafanuzi wake ulisema: “Hao wanaodaiwa kuwa waanzilishi wa Rwanda National Congress, Dk. Rudasingwa na Mshauri Condo Gervais na makamanda waandamizi wa FDLR waitwao Luteni Kanali Wilson Irategeka na Kanali Hamadi hawakuwapo Tanzania wiki iliyopita. Kwa kweli, kumbukumbu zetu hazionyeshi kwamba walizuru Tanzania katika miaka ya karibuni.
“Hakukuwa na mkutano wa aina yoyote katika makazi yoyote rasmi ya Rais Kikwete, iwe Dar es Salaam au Dodoma au popote pale.
“Rais Kikwete kamwe hakukutana na watu hao nchini Tanzania au ng’ambo. Isitoshe, katika siku ambayo News of Rwanda lilidai mkutano ulifanyika, Alhamisi ya Januari 23 mwaka huu, Rais hakuwapo nchini alikuwa Davos, Uswisi kuhudhuria Mkutano wa Jukwaa la Uchumi wa Dunia (WEF),” ilisema taarifa hiyo na kuongeza: ”tumefanya utafiti hata Idara ya Uhamiaji Tanzania haina kumbukumbu za watu hao kuingia au kuishi Tanzania”.
Taarifa ilisema Idara ya Uhamiaji Tanzania, haijawahi kutoa nyaraka zozote za kusafiria kwa raia yeyote wa Rwanda wakiwamo viongozi waliotajwa na News of Rwanda.
“Eti wanadai walisafiri kwenda Msumbiji wakitumia hati za kusafiria za Tanzania Desemba 20, 2013. Si jukumu la Tanzania kutoa hati za kusafiria za raia wa nchi nyingine,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo si kweli waasi walioweka makazi anzania wanatoa msaada wa hali na mali kwa wapiganaji wa FDLR.
“Inajulikana wazi hakuna hata mpiganaji mmoja wa FDLR katika ardhi ya Tanzania. The News of Rwanda linajua kabisa wapi walipo wapiganaji hao, kambi yao na wanakoendeshea shughuli.
“Kwa msingi huo, Tanzania inasema ripoti hiyo na nyingine zilizotolewa katika wiki za hivi karibuni na News of Rwanda, si tu kwamba si za kweli, hazina msingi na ni habari za kutunga, bali pia ni hatari na zinatishia uhusiano mzuri wa diplomasia na jamii baina ya nchi hizo mbili jirani ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),” ilisema taarifa hiyo.
Katika miezi ya mwisho ya mwaka jana, baadhi ya viongozi wa Rwanda walimkejeli Rais Kikwete baada ya kutoa ushauri wa kuitaka serikali ya nchi hiyo iwe na mazungumzo na waasi kama njia mojawapo ya kupata ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro ambao umeikumba nchi hiyo kwa miaka mingi.
Rais Kikwete alitoa ushauri huo alipokuwa akihudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Siku chache zilizopita, Umoja wa Mataifa uliionya serikali ya Rwanda kuachana na tabia ya kuzuia uhuru wa kuzungumza na kutoa maoni kwa wapinzani wa serikali ya Rais Kagame.
Onyo hilo lilitolewana Katibu Maalumu wa UN nchini Rwanda ambaye alisisitiza Rwanda inatakiwa kufungua milango ya mazungumzo.