"Haikuwa Nia ya CCM kuwafukuza Mawaziri Mizigo"


KUMEIBUKA hoja nyingi zikiwamo za kwamba iweje mawaziri ambao CCM iliwaita ‘mizigo’ wamerudishwa kwenye Baraza la Mawaziri ambalo lilifanyiwa mabadiliko na Rais wa Jamhuri ya Muungano, DK Jakaya Kikwete Jumapili Januari 19, mwaka huu na kutangazwa mbele ya waandishi wa habari na Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue?
Hoja hizo zimeibuka baada ya Sekretarieti ya CCM, Chini ya Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana, akishirikiana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na wa Siasa na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk Asha-Rose Migiro kufanya ziara ya siku 26 katika mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Njombe kuwanyooshea kidole baadhi ya mawaziri wasiowajibika katika kuondoa kero za wananchi.
Sambamba na hilo, mawaziri hao na wengine jumla yao saba waliitwa mbele ya Kamati Kuu ya CCM iliyokutana mapema, Desemba mwaka jana, kuhojiwa kutokana na utendaji wao wa kuondoa kero za wananchi kutoridhisha.
Katika mwito huo, alikuwamo aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha na sasa ndiye Waziri wa wizara hiyo, Saada Mkuya Salum kwa niaba ya Waziri wake, Dk William Mgimwa, Mungu amweke mahali pema peponi.
Wengine walikuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza; Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi; Dk Shukuru Kawambwa; Waziri wa Utumishi, Celina Kombani, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.
Katika kundi hilo, Waziri aliyeachia ngazi ni Dk Mathayo, ambaye ni kutokana na tuhumu za Oporesheni Tokomeza Ujangili kutumiwa kinyume na malengo na watendaji na kugeuza kuwa ya utesaji, ukandamizaji na ya vitendo vingine vya kinyama.
Uteuzi wake ukatenguliwa na Rais Kikwete pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi; Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsa Vuai Nahodha. Huku Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamisi Kagasheki akijiuzulu.
Kwenye baraza hilo jipya, hao wanne wameondolewa pamoja na wengine, ambapo kwenye Baraza hilo sura mpya kumi zimejitokeza na kuungana na mawaziri wengine ambao chama kiliwaona hawawajibiki vizuri ipasavyo katika kushughulikia au kutatua kero za wananchi.
Kutokana na kutowajibika huko kulibainishwa na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa inayoongozwa na Katibu Mkuu wake, Kinana ambayo tangu kuundwa kwake mwanzoni mwa mwaka jana, imekuwa ikifanya ziara mikoani kukutana na wananchi kusikiliza kero zao, kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM na kuimarisha chama mikoani.
Sekretarieti hiyo imefanya kazi nzuri na kurudisha imani ya chama kwa wananchi, lakini imefanya yote hayo kwa mujibu wa agizo la Mkutano Mkuu wa Taifa wa Nane wa CCM uliofanyika Novemba 2012 mjini Dodoma, ambao ulikiagiza chama, kiwe karibu na wananchi, kisikilize changamoto zao na kiwasemee wananchi na hasa wanyonge.
Sekretarieti imetekeleza azimio hilo na kusikiliza matatizo ya wananchi kwa kufanya ziara nyingi, ikiwamo ya mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Njombe ambapo imefanya zaidi ya mikutano 121 na kusafiri zaidi ya kilometa 6,000 katika majimbo, wilaya na mikoa hiyo, ikizungumza na wananchi, mabalozi na halmashauri za chama na kusikiliza kero zao.
Kutokana na hoja hizo kuendelea kusambaa, hasa baada ya Baraza kutangazwa ambalo ni hiari ya Rais kumteua au kutomteua yeyote, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape amezungumza na waandishi wa habari kuujulisha umma kwamba chama hakikutaka kuwaondoa madarakani mawaziri hao, bali kilitaka wajirekebishe upungufu wao.
"Haikuwa hoja ya CCM kuwafukuza mawaziri hao bali kuchukua hatua za kurekebisha upungufu... Kuwafukuza inaweza kuwa njia mojawapo ya kutatua tatizo lakini sio njia pekee.”
“CCM inaamini kwamba kurudishwa kwao mawaziri hao 'mizigo' wamepewa fursa ya kurekebisha upungufu tuliosema kwa niaba ya wananchi. Chama kinaamini kwamba mawaziri hao hawatajibweteka bali watatimiza wajibu wao na kuhakikisha wanawatumikia wananchi ambao ndio waajiri wa Serikali.
"Chama hakitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mawaziri na watendaji wengine watakaoshindwa kurekebisha upungufu na watakaoshindwa kutimiza wajibu wao vizuri. Wakumbuke kushindwa kwao kutimiza majukumu yao ni hujuma kwa Ilani ya uchaguzi ya CCM, CCM haitavumilia usaliti huo.CCM ikikaa kimya itakuwa inajinyonga yenyewe jambo ambalo hatutaruhusu kabisa," amesisitiza.
Kauli hiyo ya Katibu wa NEC, Nape inaonesha dhamira ya dhati ya CCM ya kuhakikisha mawaziri hao wanatumia fursa adimu waliyopata kuwajibika, kusikiliza kero za wananchi na kuwatembelea katika maeneo yao na kuzungumza nao ili kujua shida zao.
Ni ukweli usiopingika, Chama kikibaki kimya, wakati kilikuwa kimeanza kurudi kwenye reli kama Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, alivyokuwa anasema kwamba Kinana anarudisha chama kwenye reli, kitatoka nje ya mataruma na kufa kifo cha mende kama watendaji wa Serikali hawatawajibika katika kuondoa kero za wananchi.
Kutokana na mkakati huo wa kukirudisha chama kwenye reli, CCM haitasita kuendelea kuchukua hatua kali ndani ya chama dhidi ya mawaziri na watendaji wengine watakaoshindwa kujirekebisha na kuwajibika kutatua kero za wananchi ambao ndio mtaji wa chama na Serikali.
“Chama Cha Mapinduzi hakitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mawaziri na watendaji wengine watakaoshindwa kurekebisha mapungufu na watakaoshindwa kutimiza wajibu wao vizuri,” anasema Nape.
Ni ukweli usio na kipingamizi kwamba, kushindwa kwa watendaji hao kutimiza majukumu yao ni hujuma kwa Ilani ya uchaguzi ya CCM, CCM haitavumilia usaliti huo.”
Ili CCM ibaki madarakani kuongoza dola, lazima watendaji wake wawajibike kikamilifu kwa kusikiliza na kutatua kero za wakulima, wafugaji, wavuvi na makundi mengine katika jamii, vinginevyo itakuwa vigumu chama kushinda ushindi wa kishindo.
Nafasi hiyo adimu waliyopewa mawaziri, japo imebaki miezi 21 ili kufanyika uchaguzi mkuu mwingine, ni wazi ikitumika vizuri inaweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye jamii na kukijengea imani na kwenye chama kikashinda Uchaguzi Mkuu 2015.
"Tunawaomba Watanzania tuwape muda wateule hawa wa Rais watimize wajibu wao, lakini tusisite kusema pale tutakapoona mambo hayaendi kama tunavyotarajia. Uwajibikaji wa kweli ndio msingi wa mafanikio na maendeleo yetu," anasisitiza Nape.

HABARI LEO