WASOMI WA BAVICHA WAMUONYA ZITTO

Zitto Kabwe
Jumuiya kadhaa za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) zimeendelea kutetea uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho ya kuwavua nafasi za uongozi Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na wenzake.
Wengine waliovuliwa nafasi zao ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo Novemba 22, mwaka huu kwa tuhuma za kukisaliti chama. 


Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) limemuonya Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini kuacha kuendelea kuzungumzia uaamuzi wa Kamati Kuu kwenye vyombo vya habari kwa maelezo kuwa wanayo mambo mengi yanayomuhusu ambayo wakiyatoa hadharani yatamshushia zaidi heshima yake.

Tamko hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, John Heche, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa kwa pamoja na Baraza la Vijana Mkoa wa Mbeya na Shirikisho la Umoja wa Wanafunzi wa Elimu ya Juu wa Chadema (Chaso).

Heche alisema kuna mambo mengi kadhaa aliyoyafanya Zitto ambayo kama Bavicha itaamua kuyaanika hadharani huenda heshima aliyonayo kwenye jamii ikatoweka.

“Namsihi Zitto anyamaze, asiendelee kutumia vyombo vya habari kutaka kujitetea kwa sababu kama ataendelea kuzungumzia suala hili nasi pia tutaanika mambo yake na ninaamini kuwa ataumbuka zaidi,” alisema Heche.

Alisema kauli na matendo ya Zitto yaliwatia shaka viongozi wenzake na wanachama kwa ujumla ndani ya chama na ndiyo sababu hawakuacha kumtilia shaka na kumfuatilia kabla ya kupatikana kwa waraka unaonyesha usaliti wa wazi kwa chama hicho.

Heche alisema kuwa kitendo cha Zitto kuvuliwa madaraka kuwaumiza zaidi mahasimu wao Chama Cha Mapinduzi (CCM) badala ya wana-Chedema wenyewe kinaongeza shaka na kuwafanya waamini kuwa uamuzi uliochukuliwa na Kamati Kuu ya Chadema ulikuwa ni sahihi.

“Ukiona unafanya jambo fulani kisha ukalaumiwa na adui yako ujue kuwa uamuzi ulioufanya uko sahihi, nasi kwa kuona kuwa uamuzi wa Kamati Kuu kumvua Zitto nyadhifa zake unawaumiza zaidi wapinzani wetu wa CCM, tunaamini kuwa hatujakosea,” alisema Heche.

BAVICHA MBEYA YAUNGA MKONO

 
Kwa upande wake, Bavicha Mkoa wa Mbeya limetoa tamko la kuunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu kumvua nyadhifa zake Zitto Kabwe na kusema kuwa uamuzi huo ulifanyika kwa maslahi ya chama na Watanzania wote.

Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa wa Mbeya, Joseph Kasambala, alisema vijana wa Mkoa wa Mbeya wanaunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu kwa vile hata wao walikuwa hawaridhishwi na mwenendo wa Zitto ndani ya chama kwa muda mrefu.

“Sisi kama vijana wa Mkoa wa Mbeya tunaunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu wa kumvua nyadhifa zote ndani ya Chama Zitto Kabwe kwa sababu hata sisi tulikuwa haturidhishwi na mwenendo, kauli na matendo yake ndani ya chama,” alisema Kasambala.

Alisema Zitto kwa kipindi kirefu amekuwa akifanya vitendo ambavyo vinaonyesha wazi kukihujumu chama huku  akiwa haonekani katika baadhi ya matukio muhimu ya kukitetea chama na wananchi kwa ujumla.

Hata hivyo, Kasambala aliiomba Kamati Kuu kutumia busara zaidi kumrekebisha Zitto badala ya kumfukuza uanachama kwa sababu pamoja na makosa yake yote bado mchango wake wa kuijenga Chadema unahitajika.

CHASO MORO: NI MAAMUZI SAHIHI

 
Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (Chaso)  wa Chadema mkoani Morogoro imeunga mkono maamuzi  yaliyofikiwa na Kamati Kuu ya kuwavua uongozi Zitto na wenzake.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Chadema Mkoa, Mwenyekiti wa Chaso, Ebenezer Kwayu, alisema hayo ni maazimio ya kikao cha tarehe Novemba 30 kilichokaa kwa saa nane katika ofisi za Chadema Mkoa wa Morogoro.

Alisema uamuzi wa Kamati Kuu ulifanyika baada ya kutafakari na kubaini uwepo wa mbinu chafu za kisiasa zenye taswira ya ubinafsi kwa badhi ya viongozi ambazo zisipodhitiwa mapewa zitasababisha chama tegemewa kama Chadema kusambaratika.

“Viongozi  hawa na wengine wameonyesha taswira ya ubinafsi, siasa chafu za kuviziana na kutafutana makosa pasipo kukumbushana mapema ili kuboresha chama badala yake wamefanya hivyo wakilenga kutengeneza umaarufu ndani ya taasisi kubwa kama hii kwa faida zao binafsi, sisi wasomi Moro tunasema si sahihi na uamuzi wa Kamati Kuu ndio  sahihi,” alifafanua Kwayu.

Kwayu aliyeongozana na viongozi wa chama hicho wakiwemo wenyeviti, makatibu na makatibu wa uenezi, alisema Chadema ni chama makini na umakini wake umethibitishwa na maamuzi magumu na mazito dhidi ya hujuma zinazofanywa na baadhi ya wanachama wanaojiona miungu watu ndani ya chama.

Alisema mamuzi ya Kamati Kuu yanadhihirisha kwa Watanzania kuwa Chadema kimekomaa na kinafaa kupewa jukumu la kuongoza nchi kwa uwezo wake wa kutomwonea haya mtu, tofauti na vyama vingine kikiwemo chama tawala ambavyo vinawaingiza wananchi kwenye wakati mgumu kwa kuwa hakuna wa kumkea mwenzie kwa ufisadi na ubinafsi.

ZIARA YA DK. SLAA KIGOMA YASITISHWA

 
Uongozi wa Chadema Mkoa wa Kigoma umemuomba Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, kuahirisha ziara ya kichama mkoani humo iliyiopangwa kuanza keshokutwa.

“Mkoa uliomba Taifa lihairishe na kusogeza mbele tarehe ya ziara hiyo muhimu kwa mkoa wetu, ili Mkoa kama ngazi ya chini ya Kanda na Taifa uweze kwenda katika majimbo hayo na kuwaelimisha wanachama na wapenzi wetu juu ya kuheshimu na kuwa na nidhamu na maamuzi yatolewayo na ngazi ya juu yetu.

Hata kama yanamaumivu, “inasema sehemu ya taarifa ya Chadema Mkoa wa Kigoma ambayo imesainiwa na Mwenyekiti wake, Jafari Kasisiko, na Katibu, Msafiri Wamalwa.

Taarifa hiyo inasema kuwa uamuzi huo unatokana na kutokuwapo na uhakika wa hali ya usalama baada ya maamuzi ya Kamati Kuu.
Alisema ziara hiyo ilitarajia kuanzia Wilaya ya      Kakonko Jimbo la Buyungu na kumalizia Kanda ya Magharibi Desemba 14 mwaka huu.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo, juzi walifanya  kikao cha Baraza la Uongozi la Mkoa na kuwashirikisha viongozi wa Wilaya Kigoma Mjini,  Kusini na  Kaskasini ili kujadili na kupanga utaratibu wa ziara hiyo.

Alisema katika kikao hicho waliangalia hali ya usalama kwa sababu Katibu Mkuu ni mtu mkubwa kichama na walijadili suala hilo kwa muda wa saa tatu na viongozi waliwathibitishia kuwa hali siyo nzuri hakuna uhakika wa usalama atakapokuwa katika maeneo hayo kutokana na maamuzi ya kumvua uongozi Zitto.

Aidha, alisema Jimbo la Kasulu, Buhigwe na Muhambwe  viongozi wao walidai hali ya usalama siyo nzuri na hawawezi kumhakikishia usalama kiongozi huyo wa kitaifa.

Alisema kutokana na hali hiyo, wameamua kuwashauri viongozi wa kitaifa kuwa ni vizuri katibu mkuu akaahirisha ziara yake mkoani  Kigoma ili waweze kufanya uchunguzi wa kina kama kweli amani inaweza kuwapo.
Kasisiko alisema wameshauri makao makuu waahirishe ziara ya Dk. Slaa kwa sasa wakati wanajaribu kufanya ziara katika majimbo ya mkoa kwa kutoa elimu kuhusiana na maamuzi dhidi ya Zitto.

Alisema Kigoma ni ngome ya Chadema na kuwa baada ya muda mfupi vijana watatulia na hali itakuwa nzuri ya kumuwezesha Katibu Mkuu au kiongozi yeyote wa kitaifa kufika wakiwa na uhakika wa usalama wao.

Kuhusu maamuzi ya Kamati kuu, alisema: “Sisi kama mkoa hatujatamka chochote na hatukukusudia tutamke chochote kuhusiana na tukio hilo kwa sababu tukio limechukua utaratibu wa kawaida wa Chama.

Kikao kilichomvua madaraka Zitto Kabwe ni kikao halali cha chama, Kamati Kuu ina mamlaka na uwezo huo na sisi kama viongozi wa chini hatupaswi kuhoji kwa mujibu wa taratibu za chama chetu.”
Imeandikwa na Emmanuel Lengwa, Mbeya; Ashton Balaigwa, Morogoro na  Joctan Ngelly, Kigoma.
 
CHANZO: NIPASHE