TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI YA NDUGU ALLY O. CHITANDA
NDG: WANA HABARI: Kwanza kabisa ninawashukuru kwa kuitika wito wangu.
Jina langu naitwa ALLY OMARY CHITANDA, nimejiunga CHADEMA mwaka 2003 nikitokea NCCR –MAGEUZI.
Nyadhifa nilizowahi kuzishika na kukitumikia Chama ni:-
Kuanzia mwaka 2004- Mjumbe wa Baraza kuu Taifa nikiwakilisha vijana
Bara niliendelea kuaminiwa na Chama na kupewa kazi nyingine za
kukitumikia Chama, nimewahi kuwa Afisa wa Vijana Makao Makuu, Afisa wa
sheria na Haki za binadamu Makao Makuu, Katibu wa Kamati ya muda ya
Baraza la Vijana Taifa (BAVICHA) kwa sasa ni Mjumbe wa Mkutano Taifa
nawakilisha Nachingwea, Mwenyekiti wa Mkoa wa Lindi tangu tarehe
26/05/2013.Pia ni Afisa Mwandamizi Ofisi ya Katibu Mkuu Makao makuu Dsm.
vile vile kwa kipindi kirefu sasa nimekuwa nikifanya shuhuli ya
uandishi wa kumbukumbu za sekretarieti ya chama kama KATIBU WA
SEKRETARIETI YA KAMATI KUU. Hivyo sasa, pamoja na mambo mengine
yapo masuala nyeti na muhimu ninayoyafahamu na ikibidi kuwaarifu
watanzania kwa njia mbali mbali pindi itakaponihitaji kufanya hivyo.
Ndugu zangu wanahabari, nimewaita ili kupitia nyinyi niwaambie
Watanzania wenzaqngu juu ya hali ya kisiasa ilivyo hasa ndani ya Chama
chetu. Itakumbukwa kuwa tarehe 20-21/11/2013 Kamati kuu ya Chama ilikaa
pamoja na mambo mengine ilifanya maazimio ya kuwavua nafasi za Uongozi
ndani ya Chama alikuwa Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara Mhe. ZITTO KABWE
na Mjumbe wa Kamati kuu wa kuchaguliwa Mhe. Dr. FITILA MKUMBO, kwa kile
kilichoelezwa kuwa ni kwa sababu:-
(a) Mhe. ZITTO KABWE (Mb)
alishiriki kusaidia Wabunge watatu wa CCM kupita bila kupingwa kenye
Majimbo yao ya Uchaguzi 2010.
(b) Kuandaa mkakati waliouita
mabadiliko ya Chama 2013. Mkakati uliolenga kumuwezesha Mhe. Zitto
kushinda nafasi ya Uenyekiti wa Chama Taifa endapo angekubali kugombea.
(c) Mhe. Zitto alishindwa kutimiza majukumu yake ndani ya Chama kwa
kutoshiriki pamoja na Viongozi wenzake kwenye matukio makubwa
yaliyokikumba Chama kama:- (i) Maandamano ya Arusha. (ii) Operesheni zilzofanyika Morogoro na Iringa nk.
MAAMUZI MENGINE YA UBORESHAJI WA MAKAO:
Ni kweli kuwa pamoja na mambo mengine Baraza kuu la Chama iliridhia
pendekezo lililetwa kwake na Kamati Kuu kuhusu jambo hili.Na katika
utekelezaji wake Kamati Kuu ya juzi iliridhia kuwa, uteuzi wa
Wakurugenzi watano ambao ni:- 1. Mkurugenzi wa Oganaizesheni Mhe. Singo Kigaila Benson. 2. Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mahusiano ya ndani Mhe. John Mnyika (Mb). 3. Mkurugenzi wa Fedha na uwekezaji Mhe. Anthony Komu. 4. Mkurugenzi wa Bunge na Halmashuri Mhe. John Mrema. 5. Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama Mhe. Wilfred Lwakatale.
Uteuzi huu hauonyeshi sura ya Kitaifa Wakurugenzi wote watano ni
Wakristo kanakwamba CHADEMA hakuna Waislamu wenye uwezo wa kushika
nafasi hizo.
Lakini pia hauzingatii mgawanyo wa kijamii kwa
kuwa kati ya kurugenzi hizo sita wakurugenzi wanne kati yao wanatokea
mkoa mmoja wa kilimanjaro
Na uteuzi huu unakwenda sambamba na
kuboresha maslahi yao kwa kuongeza posho, -kutoka Tshs. 800,000/= za
awali na sasa itakuwa ni kuanzia Tshs. 1,500,000-2,500,000/= kwa
Mkurugenzi na kutoka Tshs. 6,800,000/= kwa Afisa Mwandamizi na sasa ni
Tshs.1,000,000-1,500,000/=.
Pamoja na kwamba uboreshaji
uliridhiwa, lakini katika mpango ulioridhiwa na Baraza kuu ni pamoja na
kulipa Posho kwa Makatibu wa Wilaya na Mikoa. Hawa ndio watendaji
muhimu katika Ujenzi na Uhai wa Taasisi hii lakini, hawakuangaliwa wala
kuguswa badala yake wanatakiwa kujitolea tu kwa hali na mali.
Mimi kama nilivyotangulia kusema hapo awali, kuwa niko kwa kwa miaka 10
sasa na nimeshiriki kwa kiasi kikubwa katika Ujenzi wa Chama hiki.Sioni
sababu ya kutoharakisha kulipa posho ya Mkatibu wa Wilya na Mikoa
pamoja na watendaji wengine na badala yake tunaharakisha kujilipa posho
nono sisi watendaji wa Makao Makuu, wakati hawa wa ngazi za chini
wanamaeneo makubwa ya Kiutendaji na wanafanya kazi katika mazingira
magumu kwa kujitolea hata Ofisi zao wanajitolea wenyewe.
MAAMUZI YA KAMATI KUU
Ningependa kuwaambia wanachadema na watanzania kwa ujumla, maamuzi haya
ya kamati kuu ya kuwavua uongozi zitto kabwe na dkt mkumbo ni maamuzi
ya kijuha na yanayowafanya watanzania sasa waangalie mara mbili mbili
kama hawa watu wapo makini na huo ukombozi wanaousema.
Tumekuwa tukiweka mikakati mbali mbali ya ushindi ili chama kishinde,
kwa mfano, kabla hata ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa arumeru
mashariki, wakati tu ilipobainika anaugua, chama kiliandaa mkakati wa
kushinda ubunge wa jimbo hilo na uchaguzi uliporudiwa mkakati ule
ulitumika na kushinda.
Nikiwa mtendaji wa ofisi ya katibu
mkuu, nimeshiriki pamoja na zitto kabwe na dkt Slaa kupanga mikakati
mbali mbali mizuri na mibaya kwa nchi, lakini hatukuwahi kuitwa
wasaliti, wahaini wala sina lolote baya. Ni fedheha leo mimi kuwa
sehemu ya watu wanaomuita zitto kabwe ni msaliti. Siwezi kuendelea na
ujinga huu na sipo tayari tena.
Si dhambi kumuhukumu mtu kwa kuwa anapanga mipango ya kukushinda kwenye uchaguzi, dawa ya mpinzani wako ni kumkabili.
Naomba nikiri kwamba nikiwa katibu wa sekretarieti tumekuwa
tukilazimishwa mara kadhaa kuwashawishi wajumbe wengi kutowaunga mkono
watu wenye misimamo thabiti ndani ya chama na badala yake tumekuwa
tukitumia rasilimali za chama kuwajenga wajumbe ndio.
Kwa
mfano hivi sasa tunapozungumza, wakati katibu mkuu wa chama anasema
mjadala wa zitto kabwe umefungwa rasmi, amewaagiza wakurugenzi wa chama
kuzunguza nchi nzima kusambaza waraka waliouandaa ukimchafua zitto. Hii
si sawa hata kidogo, si vema kutumia rasilimali za chama kuwanufaisha
watu binafsi kutimiza matakwa yao ya kisiasa.
Nafsi yangu haipo tayari kuendelea kuwa sehemu ya upotoshaji dhidi ya watanzania wenzangu.
Nafsi yangu inanikataza kabisa kuendelea kufumbia macho maovu yanayoendelezwa na chama changu.
Nafsi yangu imechoka kuendelea kushuhudia ubaguzi wa kidini na kikabila unaofanywa wazi wazi na viongozi wa chama changu.
Nafsi yangu imekataa sasa, haipo tayari tena kuwa kuwadi wa kuwahadaa
Watanzania kuyafikia matarajio tunayowapa ambayo kamwe hayafikiki.
Kwa kuwa siamini kwamba kuvuliwa nyadhifa kwa zitto kabwe na dkt kitila
mkumbo ni kwa sababu ya waraka wa ushindi, bali ninaamini kuvuliwa kwao
ni kutokana na hofu ya uchaguzi, ubaguzi wa kikabila na kikanda.
Hivyo basi, nikiwa na akili timamu kabisa, leo tarehe 30.11.2013
nimeamua kujivua nyadhifa zangu zote nilizokuwa nazo ndani ya chama.
Sioni tena sababu ya kuendelea kuwa MwanaCHADEMA, sioni tena sababu ya
kuwa mwenyekiti wa CHADEMA MKOA WA LINDI, sioni tena sababu ya kuwa
KATIBU WA SEKRETARIETI YA KAMATI KUU.
Kwa kuwa vipaumbele vya
chadema ni kukijenga chama mikoa ya kaskazini. Basi sisi wananchi wa
mkoa wa lindi tunawatakia kila la heri, na kwamba waendelee kukijenga
chama chao huko huko waliko.
Nashukuru wote ambao nilifanya nao kazi pamoja katika kutekeleza majukumu yangu.
Ahsante Sana
A.O. CHITANDA
0753418510
MWENYEKITI CHADEMA MKOA LINDI MJUMBE BARAZA KUU TAIFA KATIBU OFISI YA KATIBU MKUU- SEKRETARIETI