
Dodoma
Wabunge 160 wa CCM wamejiorodhesha kuomba kuitishwa kwa kikao cha Kamati ya Wabunge hao kwa lengo la kuwajadili mawaziri wanaotajwa kuwa mizigo.
Pia wabunge hao wanataka Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahaman Kinana naye awepo kwenye kikao hicho.
Mjumbe
wa Kamati ya Uongozi wa Kamati ya Wabunge wa CCM, Hussein Mussa Mzee,
alimwambia mwandishi wetu kuwa wamepokea barua iliyoambatana na orodha
ya majina ya wabunge zaidi ya 160 waliotia saini kutaka kuitishwa kwa
kikao hicho.
“Hata
kama wangesaini wabunge 10 tu tungeitisha kikao. Bahati nzuri walisaini
zaidi ya 160, kwa hiyo kikao kitaitishwa kwa kuwa ni haki yao kikanuni
kutaka kukutana,” alisema.
Alipoulizwa
kwa nini kikao hicho hakikuitishwa ndani ya wiki moja ambao ndiyo muda
wabunge hao walioutaka kabla ya Kamati Kuu ya CCM kukutana wikiendi
iliyopita, Mzee alisema hiyo lilitokana na Mwenyekiti wa Kamati ya
Wabunge wa CCM, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kutokuwapo bungeni.
Mzee
alisema pia kikao hicho kilishindwa kufanyika mara ya kwanza kutokana
na Kinana kuwa safarini Afrika Kusini ambako alihudhuria mazishi ya
Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Hata
hivyo, alisema hawezi kujua ni lini kikao hicho kitafanyika lakini
aliahidi kuwa itakuwa mara baada ya Kinana kurejea nchini.
Wiki iliyopita, gazeti hili liliandika kuhusu wabunge wa CCM kujiorodhesha ili kushinikiza kufanyika kwa kikao hicho.
Chanzo
kimoja cha kuaminika kilisema kuwa fomu hiyo iliwasilishwa katika Ofisi
ya Katibu wa Wabunge wa CCM ikiambatana na barua inayotaka kuitishwa
kwa kikao kitakachowakutanisha.
“Tuliwaomba
waitishe kikao cha wabunge wa CCM ili mawaziri ambao tunawaona
hawatimizi majukumu yao kikamilifu waweze kuhojiwa lakini wakawa
wanasuasua,” kilisema chanzo hicho.
Kikao hicho kilitakiwa kufanyika Alhamisi iliyopita ili kuwahoji mawaziri hao kabla ya kikao cha Kamati Kuu.
Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikaririwa wikiendi hii
akieleza kuwa mawaziri saba walihojiwa katika kikao cha Kamati Kuu na
kumuachia Rais Jakaya Kikwete jukumu la kuamua kuwafukuza kazi,
kuwahamisha au kuwataka kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Miongoni mwa mawaziri waliohojiwa ni Naibu Waziri wa Fedha,
Saada Mkuya na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher
Chiza, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia.
Tayari
Bunge limepitisha azimio la kumtaka Ghasia pamoja na Manaibu wake
wawili, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa kupima na kutafakari kama
wanatosha kusimamia wizara hiyo.
Kiini
cha Bunge kupitisha azimio hilo ni taarifa ya Bunge ya Hesabu za
Serikali kubainisha kuwapo wizi, ubadhirifu na mtandao wa ufisadi ndani
ya Tamisemi, kwenye halmashauri na Hazina.
Vuguvugu
linaloendelea hivi sasa la wabunge wa CCM, liliwahi kujitokeza katika
Bunge la Aprili mwaka jana na kumlazimisha Rais Kikwete kupangua Baraza
lake Mawaziri Mei 4, 2012 kwa kuondoka mawaziri sita kutokana na
taarifa za kamati za kudumu za Bunge na ile ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG).
Sefue aweka msimamo
Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amewataka mawaziri saba
wanaotuhumiwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kueleza mikakati ya
utekelezaji wa majukumu hayo kama ilivyodaiwa, badala ya kuiachia
Serikali kufanya hivyo.
Balozi
Sefue alitoa wito huo jana alipoulizwa msimamo wa Serikali baada ya
Kamati Kuu ya CCM chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete, Alhamisi na
Ijumaa iliyopita kuwahoji mawaziri hao waliodaiwa kuwa ni mzigo,
kueleza upungufu wao huku kamati hiyo ikimshauri Rais Kikwete hatua za
kuwachukulia.
“Wanaohusika
ni mawaziri kutoka wizara mojamoja hivyo wao ndiyo wanaoweza
kulizungumzia kwa undani suala hilo, ikiwa ni pamoja na mipango na
mikakati yao ya kurekebisha matatizo.”
Ghasia anena
Waziri Ghasia amesema hakuna anayepaswa kunyooshewa kidole kwa matatizo yaliyopo Tamisemi.
Akifungua
warsha ya kujadili changamoto za uongozi wa Serikali za Mitaa jana
mjini Dodoma, Ghasia alisema kwa sasa kazi kubwa iliyoko ni kurekebisha
kasoro baada ya kufanyika utafiti juu ya matatizo ya Tamisemi.
Alisema
wizara yake inashughulikia matatizo hayo baada ya kupokea ripoti ya
utafiti uliofanywa na Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute).
“Kiongozi anapaswa kuwa mbunifu anayeweza kuongoza wakati kunapokuwa na changamoto, anapaswa aone mbali zaidi ya wengine. Hatutarajii tuwe na kiongozi anayeongoza katika mazingira yasiyokuwa na changamoto kabisa,” alisema Ghasia.
“Kiongozi anapaswa kuwa mbunifu anayeweza kuongoza wakati kunapokuwa na changamoto, anapaswa aone mbali zaidi ya wengine. Hatutarajii tuwe na kiongozi anayeongoza katika mazingira yasiyokuwa na changamoto kabisa,” alisema Ghasia.