
Zitto ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, mwanzoni mwa Novemba mwaka huu
aliingia katika malumbano na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
kuhusiana na masuala ya posho, akituhumiwa na Lema kuwa anakataa posho
za vikao bungeni, lakini anapokea posho kutoka mashirika mbalimbali
nchini.
Dar es Salaam. Suala la hatma ya Naibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe ndilo lililotawala katika siku ya pili ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho na kusababisha mvutano mkali miongoni mwa wajumbe.
Pamoja
na ukweli kuwa kulikuwa na ajenda kadhaa zilizokuwa zimepangwa
kujadiliwa katika kikao hicho cha siku mbili kilichofanyika Dar es
Salaam, suala la Zitto ndilo lililochukua muda mrefu zaidi kujadiliwa.
Habari
za kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza kuwa wajumbe
waligawanyika makundi mawili, baadhi wakipendekeza Zitto avuliwe nafasi
yake ya Naibu Katibu Mkuu kwa maelezo kuwa anakwenda kinyume na
taratibu za chama hicho na wengine wakipinga hatua hiyo kwa maelezo
kuwa haina tija.
Mpaka
saa moja usiku jana gazeti hili likienda mitamboni, kikao hicho
kilikuwa bado kikiendelea na suala hilo lililokuwa chini ya ajenda ya
hali ya siasa nchini.
Mkurugenzi
wa Oganaizesheni na Uchaguzi wa chama hicho, Benson Kigaila aliahidi
kuwa taarifa rasmi ya kikao hicho ingetolewa baadaye na Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe.
Tuhuma za Zitto
Zitto
ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, mwanzoni mwa Novemba mwaka
huu aliingia katika malumbano na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
kuhusiana na masuala ya posho, akituhumiwa na Lema kuwa anakataa posho
za vikao bungeni, lakini anapokea posho kutoka mashirika mbalimbali
nchini.
Pia,
aliingia katika malumbano na chama chake baada ya kutumia kofia yake ya
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kutuhumu
vyama vya siasa kuwa hesabu zake hazikaguliwi na Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kauli
ambayo jana Kigaila aliitolea ufafanuzi na kueleza kuwa Chadema
kimekaguliwa na hesabu zake tayari zipo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Hekaheka za jana
Mvutano wa jana ulianza baada ya Mbowe kufungua kikao hicho saa 4:00 asubuhi.
Habari
kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza kuwa baadhi ya wajumbe, wakiwamo
wabunge, walitaka Zitto avuliwe nafasi aliyonayo na kuwa mwanachama wa
kawaida, huku wengine wakipinga hatua hiyo kwa maelezo kuwa Zitto
hakuwepo katika kikao hicho na kwamba alipaswa kusikilizwa.
“Baada ya hali kuwa hivyo, Mbowe alipendekeza kuwa Zitto
asijadiliwe kwa kuwa hakuwepo katika kikao hicho,” kilieleza chanzo cha
habari hizo.
Zitto alikuwa katika safari ya kikazi huko Sudan Kusini akiwa amefuatana na wajumbe wa PAC.
Taarifa
zaidi zinaeleza kuwa Zitto alitafutwa na alituma salamu kwa wajumbe wa
kikao hicho akiwaeleza kuwa alikuwa njiani na kuahidi kuwa angehudhuria
mara tu baada ya kuwasili.
“Zitto
alituma ujumbe kuwa anakuja katika kikao, kilikuwa na ajenda nyingi
lakini suala lake lilijadiliwa kwa kirefu sana,” kilieleza chanzo
chetu. Licha ya ombi la Mbowe, bado wajumbe walishinikiza kuendelea
kumjadili Zitto hivyo kusbabisha kuchelewa kujadiliwa kwa ajenda
nyingine.
Tangu
juzi, siku ya kwanza ya kikao hicho, ulinzi uliimarishwa nje ya Jengo
la Ubungo Plaza na jana walinzi wa chama hicho, Red Brigade waliwatimua
waandishi wa habari waliokaribia eneo hilo wakisema hayo ni maagizo
kutoka kwa uongozi wa juu.
Yaliyojadiliwa
Katika
ufafanuzi wake kwa waandishi wa habari jana jioni, Kigaila alisema
kikao hicho kilichoanza juzi, kimejadili mambo mbalimbali. Alisema juzi
kikao hicho kilijadili muhtasari wa vikao viwili vya dharura vya Kamati
Kuu vilivyofanyika hivi karibuni.
“Tumejadili
taarifa ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiembesamaki, Zanzibar
unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni... tunathibitisha kuwa
tutashiriki,” alisema.
“Kulikuwa
na taarifa ya hesabu za chama zilizokaguliwa na kupelekwa kwa Msajili
wa Vyama vya Siasa na taarifa za fedha za utendaji kuanzia Kamati Kuu
iliyopita mpaka Kamati Kuu ya sasa,” alisema Kigaila.
Huku
akionyesha kitabu cha ukaguzi wa fedha mwaka 2010/11 na 2011/12
alisema: “Kamati Kuu imeridhika kuwa chama kimekaguliwa na hatuna deni
kwa msajili.
Ajenda za jana
Alisema
kikao cha jana kilijadili ajenda za uboreshaji wa jengo la makao mkuu
pamoja na kupanga upya kurugenzi za chama hicho pamoja na nguvu kazi ya
makao makuu ili kuweza kutekeleza vizuri majukumu yake.
Ajenda inayoendelea hivi sasa ni ya uundaji wa programu ya `Chadema ni Msingi’, ambayo lengo lake ni kukijenga chama katika ngazi za chini kabisa. Huu ni mpango mkuu wa chama wa `Vuguvugu la Mabadiliko’ (M4C). Ajenda ya mwisho itakuwa ni kujadili hali ya kisiasa nchini.”
Ajenda inayoendelea hivi sasa ni ya uundaji wa programu ya `Chadema ni Msingi’, ambayo lengo lake ni kukijenga chama katika ngazi za chini kabisa. Huu ni mpango mkuu wa chama wa `Vuguvugu la Mabadiliko’ (M4C). Ajenda ya mwisho itakuwa ni kujadili hali ya kisiasa nchini.”
Zitto atinga usiku
Zitto
alifika katika kikao hicho jana saa 2.24 usiku akiwa na walinzi wanne
na habari kutoka ndani zinasema kwamba mara baada ya kuingia, ajenda ya
kumjadili ilirejea. Ilielezwa kwamba alipewa nafasi ya kujitetea baada
ya kusomewa ‘mashtaka’ yaliyokuwa yakimkabili.
Mwandishi
wetu aliyekuwa katika eneo hilo anasema baada ya kurejeshwa kwa agenda
hiyo malumbano makali yalizuka kwani wajumbe walikuwa wazungumza kwa
sauti za juu na jazba kiasi cha kusikika nje.