Baadhi
ya walimu wakuu wa shule za sekondari Tanzania kanda ya mashariki
kupitia umoja wao TAHOSSA wakimsikiliza ofisa elimu mkoa wa pwani hayupo
alipofungua mkutano wao mjini Kibaha.

Picha ya pamoja na baadhi ya walimu wakuu wanaounda umoja wao wa TAHOSSA Kanda ya mashariki.
Na John Gagarini, Kibaha
OFISA
Elimu Mkoa wa Pwani Yusufu Kipengele amewataka walimu mkoani humo
kuachana na tabia ya kutumia vilevi waingiapo madarasani kufundisha
kwani hali hiyo inachangia kushuka kwa kiwango cha elimu.
Imebainika
kuwa baadhi ya walimu wamekuwa wakitumia vilevi aina ya viroba kabla
ya kuingia madarasani kufundisha hali ambayo ni moja ya sababu ya
kiwango cha elimu kushuka ambapo mwalimu husika kufundisha chini ya
kiwango.
Aliyasema
hayo juzi mjini Kibaha wakati akifungua kikao cha umoja wa walimu wakuu
wa shule za sekondari Tanzania (TAHOSSA) kanda ya Mashariki na kusema
kuwa tabia kama hiyo haipaswi kufumbiwa macho na viongozi wa idara ya
elimu ili kurekebisha mwenendo wa walimu.
“Baadhi
ya walimu wamekuwa wakitumia pombe aina ya viroba jambo ambalo limekuwa
likichangia maadili kuvunjika kwa walimu na wanafunzi
wanaowafundisha,” alisema Kipengele.
Alisema
kuwa baadhi ya walimu wamekuwa wakitumia vilevi hivyo pamoja na
wanafunzi hivyo kufanya taaluma kushuka kwani walimu hao uwezo wao
unashuka na kushindwa kuwapatia kile wanachotakiwa kuwafundisha
wanafunzi.
Akijibu
baadhi ya hoja ikiwemo ya kukosa fedha kwa ajili ya wasimamizi wa
mitihani ya vitendo aliwataka kuhakikisha wanapeleka suala hilo kwenye
uongozi wa bodi ili waridhie ili wazazi wachangie sehemu ya gharama hizo
ambapo kwa upande wa serikali nayo itachangia kwa kiasi.
Awali
akimkraibisha mgeni rasmi ambaye ni ofisa elimu wa mkoa mwenyekiti wa
TAHOSSA Omary Msami alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto kubw aikiwa
ni pamoja na mitihani ya vitendo kutokuwa na fedha toka wizarani.
“Tunaomba
tupatiwe mafunzo kazini kwani walimu hawapatiwi jambo ambalo
linasababisha walimu kushindwa kwenda na wakati kwani baadhi ya mambo ya
ufundishaji yamekuwa yakibadilika,” alisema Msami.
Aidha
aliomba ukaguzi mashuleni ufanywe kila mwaka ama baada ya miaka miwili
ili kurekebisha kasoro zinazojitokeza na kuwalipia wakaguzi hao ili
kuzipunguzia mizigo shule.
Umoja huo unaundwa na mikoa ya Pwani na Morogoro ambapo kuna jumla ya shule 384 na walimu wakuu 131.