HUYU NDIYE DC ALIYEWAPANIA VIJANA

Hakika cheo ni dhamana, hivyo ni muhimu kwa wenye dhamana hiyo kujitambua na kuonyesha wanavyoweza kubeba dhamana hiyo kwa jamii husika.
Halima Dendegu, ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Tanga, mkoani Tanga anaweza kuwa mfano wa kuigwa kwa kuonyesha alivyobeba dhamana hiyo ya kuiongoza wilaya kutokana na kugeukia kundi la vijana wilayani kwake akidhamiria kuwakomboa.
Dendegu aliyeteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, Mei mwaka 2012 kuwa mkuu wa wilaya hiyo anaeleza kuwa baada ya kuingia wilayani humo alifanya utafiti na kubaini kundi kubwa la vijana likijihusisha na matumizi ya dawa za kulevya kwa sababu mbalimbali.
“Nilianza kubaini vijiwe vingi vya vijana na hawana ajira, nilipofuatilia zaidi niligundua wengi wametumbukia katika matumizi ya dawa za kulevya,”anasema Dendegu na kuongeza:
“Nilibaini vijana 867 wavulana na wasichana, walioathirika kwa matumizi ya dawa za kulevya.”
Anabainisha kuwa baada ya kuwahoji vijana hao walitoa sababu mbalimbali za kujiingiza kwenye dawa za kulevya ikiwamo kukosa ajira, makundi na kukata tama.
“Wengine walisema walishawishiwa, wapo waliosema kiingiacho mjini siyo haramu, waliokuwa wakiuza dawa hizo, hata walioshindwa kutimiza malengo yao maishani,” anasema Dendegu.
Anaongeza: “Kwa sababu hiyo, nimeanzisha kituo ili kuwatibu, kimeanza na vijana 150 na 78 kati yao wameanza matibabu wakiwamo wasichana 28.”
Anabainisha kwamba kwa kuwa lengo lake ni kuwaepusha wasirudi kwenye dawa za kulevya katika kituo hicho ameanzisha pia utoaji elimu ya ujasiriamali.
“Tayari tumebabini wenye vipaji mbalimbali, wapo wapenda mpira wa miguu, watengenezaji sabuni hata wasanii wa muziki wa kizazi kipya.”
Anasema kuwa ili kuwajenga zaidi kiafya na kuanikiza vipaji vyao, kila Jumamosi huandaliwa bonanza linaloendana na michezo mbalimbali.
“Pia nimeanzisha michuano ya mpira ‘Dendegu Cup’ litazinduliwa Juni mwaka huu ili kuibua vipaji zaidi, naamini tutatoa vijana wa kucheza timu kubwa,”anasema akidokeza kuwa hata yeye anapenda na kucheza mpira wa pete, volleyball, pia kuimba.