Dodoma. Spika wa Bunge la Wawakilishi Zanzibar na Mbunge wa Bunge maalum la Katiba, Pandu Amir Kificho amechaguliwa na wajumbe wa Bunge hilo kuwa Mwenyekiti wa muda.
Kutokana na ushindi huo Kificho sasa atakuwa na kazi kuandaa kanuni ambazo zitatumika kwa ajili ya kumchagua mwenyekiti wa kudumu wa bunge hilo na kusimamia vikao vyake.
Muda wa mwenyekiti huyo wa muda utaisha Ijumaa baada ya wajumbe kupitisha kanuni za kuendesha bunge hilo na kumchagua mwenyekiti na makamu wake.
Waliochukua fomu za kugombea nafasi hiyo ni Pandu Amiri Kificho ambaye ni spika wa Bunge la Baraza la Wawakilishi, Magdalena Rwebangira, Sadifa Juma Hamisi, David Mbatia na Profesa Costa Mahalu.
Akitangaza matokeo hayo Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashililah alisema Kificho ameshinda baada ya kupata kura 393 sawa na 69.19% ya kura 558 zilizopigwa na kuwaacha kwa mbali Costa Mahalu na Magdalena Rwebangira.