
NAIBU Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, amehojiwa na
Kamati Ndogo ya Maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuikosoa CCM
kwamba sio dhambi kutangaza nia mapema kuwania uongozi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika viwanja vya Ukumbi wa
White House baada ya kumaliza kuhojiwa, mwanasiasa huyo kijana alisema
ni vyema utaratibu huo ujulikane mapema ili kuondoa mkanganyiko usio wa
lazima unaoweza kujitokeza kwa wanaotangaza nia kabla ya wakati
kuonekana wamevunja kanuni.
Alisisitiza kuwa sio dhambi wala vibaya kutangaza nia, lakini kutumia
fedha kwa nia ya kufanya ushawishi ndiyo kosa kubwa ambalo chama
kinapaswa kuchukua hatua kikijiridhisha.
“Kwa maoni yangu naona ni vyema ukawepo utaratibu wa wale wenye nia
ya kugombea urais na nafasi nyingine, wakajitokeza mapema ili jamii
iweze kuwatafakari na kuwachambua kama wana uwezo wa kuongoza badala ya
kuibuka watu ambao jamii haiwaelewi,” alisema.
Mbali na hilo, mwanasiasa huyo kijana alisema kikao hicho hakikuwa
cha kumhoji bali kilikuwa cha kubadilishana mawazo ya namna ya
kukiimarisha chama kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015.
“Hapakuwa na mashtaka yoyote kwangu, mimi binafsi nimefurahi sana
maana tulikuwa na kikao cha kujenga chama na pia tulikuwa tunajadili
jinsi ya kuimarisha chama na nilipewa nafasi ya kutoa mawazo, nami
nimetoa mawazo yaliyolenga kuimarisha chama.
“Kati ya mambo tuliyojadili ni suala la uchaguzi wa mwaka 2015,
lakini pia mamna ya kuwapata viongozi ambao hawataweza kutumia vibaya
fedha zao kwa ajili ya kusaka nafasi za uongozi,” alisema Makamba.
Kuhusu kutajwa kwake kuwa miongoni mwa wanaotajwa kutangaza mapema kugombea urais mwakani, Makamba alisema hajatangaza nia hiyo.
Akizungumza kuhusu masuala ya rushwa, naibu waziri huyo ambaye pia ni
Mbunge wa Bumbuli, alisema kama kuna vitendo vya rushwa kwenye mchakato
wa urais, CCM inapaswa ichukue hatua kuhakikisha inapambana na vitendo
hivyo kwani sheria ya uchaguzi ya matumizi ya fedha iko wazi.
Hata hivyo, taarifa zaidi zinasema kuwa kamati hiyo inatarajia
kuendelea na kikao chake leo kwa kumhoji kada aliyesalia ambaye ni
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe baada
ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira
kuhojiwa jana jioni.
Juzi, mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye
walifika mbele ya kamati hiyo ndogo ya maadili ya CCM kutoa maelezo juu
ya tuhuma za kufanya kampeni za urais kabla ya wakati.
Mwingine aliyefika mbele ya kamati hiyo ambayo ilikuwa chini ya
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu Abdulrahman
Kinana, ni Waziri wa Nishati wa zamani na Mbunge wa Sengerema, William
Ngeleja.
Katika hatua nyingine, Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM taifa, leo
inatarajia kuanza kikao chake mjini Dodoma ambapo pamoja na mambo
mengine, kupigilia msumari msimamo wao wa kutaka serikali mbili tofauti
na mapendekezo ya rasimu ya katiba inayotaka serikali tatu.
Habari zinasema kuwa msimamo huo wa NEC ndio utakaoenezwa kwa wabunge
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wajumbe 201 walioteuliwa kuingia
kwenye Bunge Maalumu la Katiba ambalo wengi wanatoka CCM.