
RAIS Jakaya Kikwete ameitaka Jumuia ya Kimataifa kusaidia kukomesha
na kufunga masoko ya pembe za tembo na faru kama moja ya njia za
kukomesha mauaji na biashara haramu ya wanyamapori hawa.
Akizungumza jana kwenye mkutano wa kimataifa wa kukabiliana na
ujangili na biashara haramu ya pembe za tembo kwenye jumba la Lancaster
jijini London, Uingereza, Rais Kikwete alisema kuwa bila kufunga masoko
hayo kazi ya kudhibiti ujangili na mauaji ya wanyamapori hao itakuwa
ngumu.
Rais Kikwete alikuwa mmoja wa viongozi wa Afrika ambao walizungumza
kwenye ufunguzi wa mkutano huo uliohudhuriwa na wakuu wa serikali na
nchi pamoja na wawakilishi wa nchi 60 duniani.
Mkutano huo umeandaliwa na Serikali ya Uingereza kwa ombi la mtoto wa malkia, Prince Charles.
Mbali na Rais Kikwete, viongozi wengine wa Afrika walioshiriki
mkutano huo na kuzungumza ni pamoja na Rais wa Botswana, Jenerali Khama
Iam Khama; Rais wa Gabon, Ali Omar Bongo na Rais wa Chad, Idrissa Deby.
Ethiopia iliwakilishwa na waziri.
Rais Kikwete amewaambia mamia ya wajumbe wa mkutano huo: “Mwisho,
nataka kuiomba jumuia ya kimataifa kuweka msimamo na kusaidia kukomesha
biashara ya pembe za tembo na faru duniani. Kama hili litafanyika tembo
na faru watakuwa salama.”
Ameongeza: “Wakati CITES ilipopiga marufuku biashara ya
pembe za tembo mwaka 1989, hali hiyo ilisaidia kuongezeka kwa idadi ya
tembo duniani. Naamini kuwa kama biashara hiyo itapigwa marufuku tena
leo, matokeo yatakuwa yale yale. Maisha ya tembo na faru wengi
yataokolewa na hatutakuwa na haja ya kuwa na wasiwasi.”
Rais Kikwete pia ametoa mapendekezo mengine makuu manne kama njia ya
kukabiliana na ujangili na biashara haramu ya pembe za ndovu, ikiwa ni
pamoja na ahadi kwamba serikali itaendelea kuongeza nguvukazi ya maofisa
na askari wanyamapori na kuhakikisha kuwa maofisa na askari hao
wanapata mafunzo mwafaka ya kuifanya kazi hiyo.
Wakati huo huo, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)
limeitaka Tanzania kuanzisha haraka awamu ya pili ya Operesheni Tokomeza
yenye lengo la kukabiliana na kasi kubwa ya ujangili na mauaji ya
wanyamapori katika Tanzania.
Shirika hilo limesema kuwa linatambua na kupongeza juhudi
zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kupambana na ujangili, ikiwa ni
pamoja na kuanzisha Operesheni Tokomeza kupambana na balaa la uwindaji
haramu wa wanyamapori na biashara haramu ya meno ya tembo.
Msimamo na pongezi hizo za UNDP zimetolewa juzi na Mkuu wa Shirika
hilo la Umoja wa Mataifa, Hellen Clark wakati alipozungumza kwenye
mkutano huo wa kimataifa wa kupambana na ujangili na biashara haramu ya
meno ya tembo.
Katika hatua nyingine, Uingereza imemwalika Rais Kikwete kwa ziara
rasmi kutembelea nchi hiyo kwenye sehemu ya kwanza ya mwaka huu, na
amekubali mwaliko huo.
“Tunakualika rasmi na kukuomba Mheshimiwa Rais uwe mgeni wa Serikali
ya Uingereza wakati wowote katika sehemu ya kwanza ya mwaka huu,” Waziri
wa Mambo ya Nje na Jumuia ya Madola wa Uingereza, William Hague
amemwambia Rais Kikwete ambaye naye ameukubali mwaliko huo.
Waziri Hague ametangaza hatua hiyo ya Uingereza kumwalika Rais
Kikwete alipokutana na kufanya mazungumzo na waziri huyo kwenye makao
makuu ya wizara hiyo jijini London.