Watu 29 wahukumia kifungo cha miaka 3 jela kutokana na vurugu za nani anaruhusiwa kuchinja zilizotokea mwaka jana




Mahakama ya Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya, imewahukumu watu 29 kifungo cha miaka mitatu jela kila mmoja ama kulipa faini ya Sh400,000 baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kuandamana bila kibali na kuvunja nyumba za ibada wakati wa vurugu za kugombea kuchinja katika Mji wa Tunduma wilayani Momba mwaka jana. 
 
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Rahimu Mushi akisoma hukumu hiyo alisema mahakama yake imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na kwamba wanatiwa hatinani kwa matendo yao.
 
Hata hivyo ni washtakiwa watano tu kati yao waliokwenda jela, huku wengine 24 wakilipa faini.
 
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Februari 4 mwaka jana, wakishtakiwa kwa makosa sita ya kuandamana bila kibali, kufanya vurugu, kuharibu mali, kuchoma matairi barabarani na kumpiga askari.
 
Mushi alisema kulingana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, mahakama imeridhika na kuwatia hatiani washitakiwa kwa makosa manne ya kuandamana bila kibali, kuchoma matairi barabarani, kuvunja nyumba ya ibada nyumba ya askari na kumjeruhi askari.