POLISI Kanda Maalum ya Dar es Salaam imetangaza leo kufanya doria kwa kutumia helikopta ili kuangalia hali ya usalama katika jiji hilo katika sikukuu ya Mwaka Mpya.
Aidha, imepanga kushirikiana na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama, ikiwa ni pamoja na Kikosi cha Zimamoto na uokoaji na vikundi vya ulinzi shirikishi kuhakikisha kunakuwepo udhibiti wa matukio ya uhalifu au fujo zinazoweza kujitokeza.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema pia wamejipanga kutumia Kikosi cha FFU kukijumuisha na askari na magari ya washawasha na askari wa mbwa na farasi, kukabili uhalifu.
Alisema vikosi vyote vya Polisi, vikihusisha askari wa vyeo vyote, vimekuwa barabarani saa sita kabla ya Mwaka Mpya, vikifanya doria, ambapo pia wakaguzi wa tarafa wamehusika.
Alisema kutokana na sababu za kiusalama na matishio mbalimbali katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki, waliamua kupiga marufuku upigaji fataki katika Mkesha wa Mwaka Mpya.
Aidha, alisema Kikosi cha Polisi Wanamaji kitafanya doria kwenye fukwe za bahari na maeneo yote ya bahari jijini Dar es Salaam. Pia, ulinzi umewekwa katika fukwe hizo kwa kuweka vituo vya polisi vya muda, vinavyohamishika ili kutoa msaada wa haraka unapohitajika.
Alishauri wananchi kusherehekea Sikukuu ya Mwaka Mpya katika ngazi ya familia au kukusanyika katika mitaa kwa amani, bila kuvunja sheria.