Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick UtohDodoma. Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utoh amesema kuwa Serikali ya Tanzania iko hoi kifedha hivyo Bunge na Serikali lazima wajitathmini.
Hata hivyo, alisema kuwa wanayo matumaini makubwa
kutokana na ushauri mwingi ambao umekuwa ukitolewa na ofisi yake
kufanyiwa kazi ikiwemo mfumo wa utayarishaji wa bajeti za Serikali
kuanzia mwaka 2013/14.
Utoh alitoa kauli hiyo jana katika ukumbi wa St
Gasper nje kidogo ya Mji wa Dodoma kwenye mkutano wa pili wa baraza la
wafanyakazi wa ukaguzi nchini.
Mkutano huo uliwajumuisha wajumbe wawakilishi
kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na wataalamu wengine na
ulilenga kuendelea hadi leo ambapo CAG ndiye mwenyekiti wa mkutano huo.
CAG alisema katika maswali hayo kuna changamoto na matatizo makubwa ambayo yanatakiwa kutafutiwa ufumbuzi.
Alisema ni vyema Serikali ikaangalia kwa makini
matumizi yake ikiwemo kusimamia kwa nguvu vyanzo vya mapato ili kuondoa
changamoto hizo.
Kuhusu ofisi yake alisema bado inakabiliwa na
changamoto kubwa ya watumishi jambo linalosababisha ufanisi katika
utendaji kazi kuwa wa chini ya kiwango.
Alitaja kwa Serikali za Mitaa pekee wanahitajika
wakaguzi 500 kwa nchi nzima, lakini waliopo hivi sasa ni wakaguzi 278
hivyo kuwa na upungufu wa watumishi 222.
Kwa upande wa wafanyakazi wa ofisi hiyo kwa
ujumla, alisema wako wakaguzi 802 ukilinganisha na wakaguzi 531
waliokuwepo mwaka 2010, aidha kati yao 81 ni wakaguzi wa Umoja wa
Mataifa ambao wanatakiwa kuongezwa wengine 69 ili kufikia 150.
Akizungumza katika Mkutano huo, Katibu Mkuu
Utumishi, George Yambesi alisifu kuwa ofisi ya CAG imesaidia kwa kiasi
kikubwa katika utendaji wa watumishi pamoja na kupunguza hati chafu na
zenye shaka ndani ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.
Hata hivyo, Katibu Mkuu alisema bado kuna
changamoto kubwa kwa wakaguzi kwani baadhi yao wamekuwa si waaminifu
katika shughuli zao ikiwemo kupokea rushwa.
“Serikali itaendelea kupokea ushauri mzuri wa CAG,
lakini napenda mfahamu kuwa lazima mzingatie maadili yenu na wakaguzi
wawe wasafi kwa tabia kuliko wanaowakagua kwani ziko tetesi kuwa baadhi
yenu ni wala rushwa,” alisema Yambesi.
Alimtaka CAG kuendelea kutoa ushauri wa kitaalamu namna ambavyo Serikali itaboresha makusanyo yake na matumizi na kuahidi kuongeza idadi ya wakaguzi pale uchumi wa nchi utakaporuhusu.
Alimtaka CAG kuendelea kutoa ushauri wa kitaalamu namna ambavyo Serikali itaboresha makusanyo yake na matumizi na kuahidi kuongeza idadi ya wakaguzi pale uchumi wa nchi utakaporuhusu.