Mrema aandika vitabu viwili

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema ametoa vitabu viwili kuelezea utekelezaji na mikakati yake katika kutetea wananchi wa Jimbo la Vunjo anaoongoza.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mrema alisema maudhui ya vitabu hivyo ni kueleza mikakati yake katika kuwatetea wananchi wa Vunjo kuwakwamua na kero mbalimbali zinazowakabili.
Mrema alisema kitabu cha kwanza kimelenga kuelezea hatima ya wakulima wa kahawa, ambao ndiyo walio wengi Vunjo.
Katika kitabu hicho, Mrema amehoji sababu za Chama Kikuu cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU) kuendelea kukopa kahawa za wakulima, kushindwa kuwalipa mabaki, ushuru na nyongeza za wakulima.
Mrema katika kitabu hicho vilevile amehoji iwapo kuna ukweli wa KNCU kuidai Serikali fedha za fidia zinazotokana na mdororo wa uchumi mwaka 2008/09, au kinawahadaa wananchi.
Katika kitabu cha pili, Mrema ameelezea alichokiita ukweli kuhusu kiwanda kinachojengwa eneo la njia panda ya Himo jimboni humo, ambacho kumekuwa katika mgogoro baina ya wananchi na mwekezaji.
Mrema alisema kumekuwa na madai kuwa yeye (Mrema), anamzuia mwekezaji kujenga kiwanda eneo la Himo ili wananchi wakose ajira na kwamba ameamua kutumia kitabu hicho kueleza ukweli.
Ndani ya kitabu hicho, zipo barua za malalamiko ya wananchi kwenda kwa Waziri Mkuu na wakipinga ujenzi huo.
na uendeshaji wa kiwanda hicho kinachodaiwa kimejengwa katika eneo la makazi ya watu huku mwekezaji akikiuka sheria na kujenga bila kibali.
Vile vile vipo vielelezo toka wizara ya ardhi vikikubaliana na malalamiko ya wananchi na vinavyomuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya Moshi ahakikishe kiwanda hicho hakijengwi na kama kimejengwa basi kisimamishwe na mwekezaji alipe faini
Mrema anasema yeye kama mwakilishi wa wananchi hao atahakikisha anawasemea wananchi wake na kupambana kukabiliana na kero zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo