Baadhi watwangana nje ya Mahakama Kuu kabla ya kesi ya Zitto kuanza kusikilizwa

 
Na Beda Msimbe — WAFUASI wa CHADEMA, leo waligeuza eneo la Mahakama Kuu ni la kuoneshana ubabe baada ya kukunjana na kupigana kabla ya kesi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kuanza kusikilizwa Mahakamani hapo.

Kabla hata hawajakunjana wafuasi hao walitumia nafasi hiyo kumzomea mbunge huyo wakidai kesi aliyofungua dhidi ya 
chama hicho inawacheleweshea muda.

Vurugu hizo zilianza saa 3 asubuhi baada ya Mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi saa 4, ndipo wafuasi hao walipomfuata Zitto kumfanyia fujo jambo lililosababisha askari wamchukue na kumhifadhi katika chumba maalumu kwa usalama wake.

Wakili wa CHADEMA, Tundu Lissu aliwaita wanachama hao na kuwasihi watulie wasikilize walichoitiwa mahakamani hapo ili wasizuiwe kuingia mahakamani, hata hivyo kwa ujasiri saa 5.50 wafuasi hao walianza tena vurugu na kutaka kumpiga askari kanzu wakidai anawarekodi.

Balaa likawa kubwa zaidi pale mmoja wa wana CHADEMA alipomtetea askari huyo, kwani kibao kikamgeukia na kutandikwa hadi kumchaniwa shati.

Zitto amefungua kesi dhidi ya Baraza la Wadhamini la Chama hicho na Katibu Mkuu, Wilibrod Slaa, akiiomba Mahakama itoe zuio la muda la Kamati Kuu kutojadili suala la uanachama wake hadi rufaa yake itakaposikilizwa katika Baraza Kuu la Chama.

---- MWISHO WA NUKUU YA TAARIFA KUTOKA KWA Beda Msimbe -----

Nalo Gazeti la UHURU limeandika ifuatavyo:

WAFUASI wa CHADEMA na wale wanaodaiwa wa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, leo walitwangana makonde nje ya viunga vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

Hali hiyo ilijitokeza kabla na baada ya Jaji John Utamwa kusikiliza maombi ya Zitto, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kuiomba mahakama itoe zuio la muda kwa Kamati Kuu ya chama hicho na chombo chochote kumjadili na kuamua kuhusu uanachama wake.

Vurugu hizo zilianza mapema saa 3.30 asubuhi, baada ya mahakama kutamka kwamba maombi ya Zitto ambayo amefungua dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa CHADEMA na Katibu Mkuu wa chama hicho, yatasikilizwa saa 4.30 asubuhi. Wafuasi wa chama hicho, ambao walikuwa wamefurika  walianza kumzomea Zitto, kwa madai ni fisadi na kwamba kesi aliyofungua inawapotezea muda.

Kutokana na hali hiyo, Zitto, aliyekuwa akilindwa na mabaunsa wawili na vijana wengine wawili, aliondoka eneo hilo na kwenda kukaa katika chumba maalumu kwa usalama wake.

Hali hiyo ilisababisha Wakili wa CHADEMA, Tundu Lissu, kuwaita wanachama hao na kuwasihi watulie wasikilize walichoitiwa mahakamani hapo ili wasizuiwe kuingia mahakamani.

Hata hivyo, ilipotimia saa 5:50 asubuhi, wafuasi hao walianzisha fujo tena na kutaka kumpiga mtu mmoja kwa madai anawarekodi, jambo lililomlazimu mmoja wa askari kanzu kuingilia kati na kumuokoa mtu huyo.

Zitto amefungua kesi dhidi ya Baraza la Wadhamini la Chama hicho na Katibu Mkuu, Dk. Willbrod Slaa, akiiomba Mahakama itoe zuio la muda la Kamati Kuu kujadili suala la uanachama wake hadi rufani yake itakaposikilizwa katika Baraza Kuu la Chama.

Aidha anaomba Mahakama imwamuru Dk. Slaa ampe nakala za taarifa za vikao vilivyomvua uangozi ili akate rufaa.
Maombi ya Zitto, anayewakilishwa na Wakili Albert Msando, diwani wa CHADEMA, kata ya Mabogini, yalianza kusikilizwa saa 6.53 mchana, mbele ya Jaji John Utamwa.

Msando aliiomba mahakama itoe zuio la muda la Kamati Kuu na vikao vingine vya chama kutojadili suala la uanachama wa Zitto hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Juzi Mahakama iliamuru Kamati Kuu kutojadili suala la uanachama wa Zitto katika Mkutano uliofanyika leo baada ya kutupilia mbali pingamizi la CHADEMA na kukubali ombi la Zitto.

Akiwasilisha hoja zake Wakili Msando aliomba zuio hilo litolewe hadi Zitto atakapopata nafasi ya kuwasilisha rufaa yake ya kupinga uamuzi wa kumvua uongozi katika Chama, uliotolewa katika kikao kilichofanyika Novemba 22, mwaka jana