Uongozi
wa klabu ya Young Africans SC umempatia taarifa (Notice) ya siku ya
thelathini (30) kocha mkuu mholanzi Ernie Brandts juu ya kusitisha mkataba
wake kuanzia jana Disemba 22 mwaka huu.
Maamuzi hayo yanafuatia muenendo wa matokeo mabaya katika michezo iliyopita
ya Ligi Kuu, kirafiki na bonanza la Nani Mtani Jembe dhidi ya Simba SC
mwishoni mwa wiki.
Hatua ya Young Africans SC kusitisha huduma na Brandts isichukuliwe kama
chuki bali ni moja ya sehemu ya
kuhakikisha tunaboresha benchi la ufundi ili
tuweze kupata matokeo mazuri katika Mashindano yanayotukabili.
Ukitazama uwezo wa mchezaji mmoja mmoja wa Yanga
SC na wapinzani wetu, na soka tulilocheza kwenye mchezo wa mwishoni mwa wiki
kwa kweli ni dhahiri mwalimu amefikia mwisho kimbinu na hana njia mbadala.
Young Africans SC imekua ikicheza chini ya
kiwango katika michezo ya Ligi Kuu hali iliyoplekea kupata ushindi kwa tabu
na wakati mwingine timu kupoteza pointi.
Kufuatia kupewa taarifa ya siku 30, Brandts
ataamua mwenyewe kama ataendelea kusimamia mazoezi ya timu au kuondoka moja
kwa moja kabla ya muda huo ukiwa haujakamilika.
Ikiwa Brandts ataondoka mapema timu itaendelea na
mazoezi kama kawaida katika kila siku asubuhi katika uwanja wa bora
kijitonyama kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na mashindano ya
kimataifa chini ya kocha msaidizi Fred Felix “Minziro”.
Ili kuhakikisha timu inafanya vizuri katika
mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom na mashindano ya kimataifa uongozi
unakamilisha maandalizi ya safari ya kambi nje ya nchi na taratibu zote
zitakapokamilika tutawajulisha.
Aidha uongozi upo katika mchakato wa kumapata
mrithi wa Brandts ambaye ataungana na timu kwa ajili ya maandalizi ya
mzunguko wa pili na Mashindano ya klabu Bingwa Afrika.
Mwisho tunawaomba wanachama, wapenzi na washabiki
wa Yanga wasivunjike moyo kufuatia matokeo ya bonanza mwishoni mwa wiki,
uongozi unajipanga kuhakikisha timu inaimarika kwenye benchi la ufundi na
kurudisha furaha katika mzunguko wa pili wa VPL.
Abdallah Bin Kleb
Mwenyekiti - Kamati ya Mashindano
Young Africans Sports Club.
DAR ES SALAAM
23 Disemba, 2013 |