TAMBWE.  

Mahasimu wa kihistoria katika soka la Tanzania, Simba na Yanga leo zitashuka uwanjani katika pambano la hisani la ‘Nani Mtani Jembe’ litakalopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Simba na Yanga zinakutana katika mchezo huo, huku ikiwa ikiwa imepita miezi miezi miwili tu tangu iliposhuhudiwa sare ya mabao 3-3 ya timu hizo katika pambano la  Ligi Kuu lililopigwa Oktoba 20 kwenye uwanja huohuo.
Hata hivyo, tofauti na mchezo baina ya timu hizo uliotangulia, mikwaju ya penalti itatumia kuamua mshindi endapo dakika 90 zitakamilika kwa sare.
Vikosi
Timu hizi  zitaingia uwanjani zikiwa na baadhi ya sura mpya za wachezaji waliosajiliwa wakati wa dirisha dogo la usajili, ambapo Yanga imewanasa nyota wawili wa  zamani wa Simba, kipa Juma Kaseja na mshambuliaji Emmanuel Okwi, pamoja na kiungo wa Ruvu Shooting, Hassani Dilunga.
Nayo, Simba imeboresha kikosi chake kwa kuwasajili makipa wa zamani wa Yanga, Ivo Mapunda na Yaw Berko, kiungo Awadh Juma aliyemaliza mkataba Mtibwa Sugar na  mshambuliaji wa Ally Badru kutoka Suez Canal ya Misri.Isitoshe, Simba itakayocheza dhidi ya Yanga leo itakuwa chini ya benchi jipya la ufundi litakalokuwa na kocha mkuu Zdravko Lugarusic na msaidizi wake Suleiman Matola ambayo walichukua na nafasi za  Abdallah Kibadeni na Jamhuri Kihwelo waliofungashiwa virago.
Uhalisia wa mambo
Yanga iliyokuwa imepiga kambi kwenye Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam itaingia uwanjani ikiwa inajiamini zaidi kutokana na kuwa na kikosi chenye wachezaji muhimu wanaozitumikia nchi tofauti za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kwa upande wa Simba ambayo ilijichimbia kambini Visiwani Zanzibar, ni wazi itajitupa uwanjani, lakini ikiwa na unyonge unaotokana na mgogoro wa kiuongozi unaoendelea kati ya mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Rage na kamati yake ya utendaji.
Kocha wa Yanga, Mdachi Ernest Brandts akiuzungumzia mchezo huo alisema kikosi chake kipo tayari kukabiliana na Simba na kuvuna matokeo ya ushindi.
“Tumefanya maandalizi ya  kutosha kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi (leo), sina wasiwasi na ubora  wa kikosi changu nina matumaini ya kuibuka na ushindi,” alisema Brandts.
Naye Lugarusic ambaye huo utakuwa mchezo wake wa kwanza dhidi ya Yanga alisema kikosi chake kimeiva na kitawashangaza wapinzani wake.
 “Najua Yanga wanajiamini sana, lakini mimi nasema wanakosea, itakuwa ni mechi nzuri na yenye ushindani,” alisema Lugarusic raia wa Mcrotia.