MWENYEKITI wa Simba, Ismail Rage amesema yupo
tayari kujiuzulu uenyekiti wa klabu hiyo, lakini akasisitiza hilo
lifanywe na wajumbe wote wa kamati ya Utendaji.
Kwa takriban mwezi sasa hali imekuwa si shwari ndani ya Simba, baada
ya baadhi ya wajumbe wa kamati ya Utendaji wakiongozwa na Kaimu makamu
mwenyekiti, Joseph Itang’are ‘Kinesi’ kumsimamisha Rage kwa tuhuma
mbalimbali.
Hata hivyo, Rage alikataa hatua hiyo na kusema kwamba yeye ni
Mwenyekiti halali wa Simba, pamoja na hilo Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) lilimtaka Rage kuitisha mkutano wa dharura wa wanachama ili
kutatua tatizo hilo, lakini Rage aligoma na kusisitiza kuwa endapo TFF
itamlazimisha kufanya hivyo atajiuzulu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Rage ambaye hakuwepo nchini kwa
takribani wiki tatu zilizopita, alisema hali ilivyo kwenye kamati ya
utendaji hawawezi kufanya kazi pamoja hivyo ili kuinusuru Simba ni bora
wajiuzulu wote kisha uchaguzi uitishwe mapema Januari na wanaoitakia
mema klabu hiyo kugombea.
Rage alisema kwanza hana sababu ya kujiuzulu wala kuitisha mkutano
wa dharura kwa sababu wanachama wanaompigia kelele ni wa tawi la Mpira
pesa pekee.
“Haiwezekani katika matawi 78 tawi moja tu kila siku wanaongea,
wangeongea matawi 78 kidogo ningeshtuka, mimi nimechaguliwa na watu
1,820 sasa tawi la Mpira pesa sijui lina watu 204 sijui 100 ila hata
sielewi lina watu wangapi,haliwezi kunipa taabu,’… “Sina mpango wa
kuitisha mkutano wa dharura kama hali itaendelea hivi ya kutoelewana
njia nyepesi ninayoona mwanangu (akimaanisha mwandishi aliyezungumza
naye) ni kuitisha mkutano wa uchaguzi Januari kabla ya tarehe 27, ili
upatikane uongozi mpya kuanzia Mwenyekiti na wajumbe wa kamati ya
utendaji”.
“Tusidanganyane bwana, kamati ya utendaji hatuwezi kufanya kazi
pamoja kutokana na haya yaliyotokea, ninachokifanya ni kupitia vizuri
katiba inasemaje kisha nitaandika barua ya kamati ya utendaji
kujiuzulu, kisha tuitishe uchaguzi Januari,” alisema Rage.
Aidha Rage alisema, pia anasubiri uamuzi wa TFF kuhusu malalamiko
yake maana aliandika barua kuomba kamati ipitie maamuzi yake ya mwanzo
baada ya kuona kulikuwa na dosari, na kwamba kama wakirekebisha dosari
alizoziona, atakuwa tayari kufuata maagizo yao.
“Mimi binafsi siwezi kufanya kazi na kamati ambayo tayari
ilishanituhumu na kunisimamisha, kwa hiyo tayari hawana imani na mimi,
sasa mimi imani na wao natoa wapi, kwa hiyo tutakuwa hatuwatendei haki
wanachama wa Simba. Sasa ili tuonekane wote tunafuata maadili basi ni
vyema kuanzia Mwenyekiti na Wajumbe wote wa kamati ya utendaji
tukajiuzulu, tukaitisha mkutano wa uchaguzi ili kuiokoa klabu yetu ili
ipate mafanikio makubwa”.