
Kigoma/Singida.Polisi mkoani Kigoma, imemshauri, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Wilbrod Slaa kusitisha ziara zake mkoani Kigoma kwa sababu za kiusalama.
Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Zedekia Makunja alisema jana: “Ni
ushauri tu tunatoa kwa Dk Slaa kwamba anaweza kuahirisha kutokana na
hali ilivyo hapa.” Hata hivyo, Kamanda Makunja alisema pamoja na yote
hayo bado Polisi mkoani, Kigoma imejipanga imara kukabiliana na vurugu
zozote zinazoweza kutokea katika ziara hiyo.
Lakini
Dk Slaa alipoulizwa kuhusu ushauri huo alisema hawezi kufuta ziara hiyo
na kusema hahofii chochote. Alisema na alishafahamu siku nyingi kuwa
hayo yanayotokea. Juzi, vijana mbalimbali waliandamana kwa pikipiki na
wengine wakitembea kwa mguu huku wakiwa na mabango kupinga ziara ya Dk
Slaa Kigoma. Anatarajiwa kuwasili Kigoma Kaskazini keshokutwa.
Hatua
hiyo ya kupinga ziara hiyo, imetokana na Kamati Kuu ya Chadema kumvua
madaraka aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ambaye ni
mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Wakizungumza
baada ya maandamano yao yaliyoanzia Kijiji cha Mwandiga kilichopo
Kigoma Kaskazini hadi Uwanja wa Mwanga Center, Kigoma, vijana hao
walisema kundi hilo halimuungi mkono Dk Slaa.
Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya Chadema katika Kijiji cha Mwandiga, Mtoro Mvunye
alisema: “Tumetoa wito kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Issa
Machibya na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma (RPC) Fraser Kashai
kusitisha ziara hiyo mara moja.”
Akizungumza
baada ya kupokea maandamano hayo juzi, Mvunye alisema hawataki kumwona
Dk Slaa akifika katika Kijiji cha Mwandiga, Ujiji na Mwanga.
“Kwanza
nampongeza Mkuu wa Mkoa na RPC kwa kusimamia vizuri maendeleo ya
Kigoma, lakini nataka niwaeleze kwamba endapo hawatachukua hatua ya
kumzuia Dk Slaa kuja hapa Kigoma, hawa watu wanatudharau sana sisi wa
Kaskazini,” alisema Mvunye.
Alitoa
wito kwa wanachama wa Chadema kutowapigia kura kuwachagua viongozi wote
wa mikoa na majimbo walioonyesha kutomuunga mkono Zitto katika sakata
hilo ambalo limesababisha mgawanyiko kwa baadhi ya mikoa.
Mjini
Singida, Baraza la Uongozi mkoani Singida, limemtaka aliyekuwa
Mwenyekiti Chadema Mkoa huo, Wilfred Kitundu kuomba radhi ndani ya siku
14 kutokana na kutoa taarifa ya uongo, uzushi na upotoshaji mkubwa
wakati akitangaza kujiuzulu nafasi yake hiyo. Taarifa ya Baraza la
Uongozi ilisema asipotekeleza agizo hilo, atavuliwa uanachama. Akisoma
taarifa hiyo, Kaimu Mwenyekiti, Shaaban Limu alisema tuhuma
zilizotolewa na Kitundu kuwa uamuzi uliotolewa na Kamati Kuu ya kuwavua
uongozi kina Zitto na wenzake ni za kipuuzi ni zake binafsi na si za
Chadema.
Vurugu zavunja mkutano wa Dk Slaa
Vurugu
kubwa zilizuka jana na kusababisha mkutano wa Dk Wilbrod Slaa uliokuwa
ukifanyika kwenye Uwanja wa Kigalamo, Kasulu kuvunjika.
Mkutano huo ulivunjika baada ya polisi kufyatua mabomu ya kutoa
machozi kwa kundi la vijana waliokuwa wakifanya vurugu kwa kuwarushia
mawe wanachama na wapenzi wa chama hicho waliokuwa wakimsikiliza Dk
Slaa.
Vurugu hizo zilianza baada ya Dk Slaa kumaliza kuhutubia na kuruhusu watu kuuliza maswali.
Polisi
walichukua hatua hiyo baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya.
Walifyatua mabomu kutawanya kundi hilo na kumteremsha Dk Slaa
harakaharaka jukwaani na kuingizwa kwenye gari na kuondoka chini ya
ulinzi vijana wa chama hicho, Red Brigade.
Imeandikwa na Frederick Katulanda, Thomas Kayanda na Gasper Andrew.