Ikiwa imebaki miaka miwili kufanyika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015,
vyama vya siasa vimeanza kujiandaa ili kuhakikisha vinashinda uchaguzi
huo na kushika dola.
Miongoni mwa vyama vinavyojiandaa, ni Chadema
ambacho kimeanza kujitazama na kuwajibishana ili kujiweka sawa, kisha
kuunda timu madhubuti ya ushindi mwaka 2015.
Kamati Kuu ya Chadema, hivi karibuni iliwavua
nyadhifa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe na
Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo kwa tuhuma za kuendesha mambo
yanayodaiwa kutaka kukisambaratisha
.
.
Kuchukua uamuzi kama huo kwa Chadema si mara ya
kwanza. Itakumbukwa kwamba shoka kama hilo liliwahi kumwangukia
aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wake, marehemu Chacha Wangwe aliyevuliwa
wadhifa wake na mauti kumkuta siku chache baadaye.
Rungu kama hilo liliwahi kumwangukia aliyekuwa
Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Amani Kaborou ambaye sasa ni Mwenyekiti
wa CCM Mkoa wa Kigoma. Pia David Kafulila alivuliwa cheo akatimkia
NCCR-Mageuzi.
Mapema mwaka huu, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la
Vijana Chadema (Bavicha), Juliana Shonza na wenzake akiwemo Mtela
Mwampamba na Habib Mchange walifukuzwa uanachama katika chama hicho
kutokana na kutuhumiwa kukisaliti.
Inaweza kuelezwa kuwa hiyo ni migogoro, lakini pia
ni uamuzi mgumu wa kujisafisha na kujiweka sawa ili kuingia katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 bila vikwazo.
Hata hivyo, kwa baadhi ya vyama vya siasa suala la
kuchukua uamuzi mgumu wa kujisafisha limekuwa jambo gumu na uamuzi huu
wa Chadema unapingwa kwa sababu mbalimbali, ikiwamo ya kukiuka misingi
ya demokrasia.
Mathalan, Chama Cha Mapinduzi (CCM), tangu
kilipotangaza kaulimbiu yake ya kujivua gamba mwaka 2011 mpaka sasa
hakijafanya lolote, badala yake kimebaki tu kulalamika jukwaani na
kushutumiana wao kwa wao.
Ukiacha Mwakilishi wa Kiembesamaki, Mansour Yussuf
Himid aliyetimuliwa kwa madai ya kushindwa kutekeleza wajibu kwa
wanachama na kutokutekeleza ilani ya chama hicho ya mwaka 2010/2015,
hakuna kumbukumbu nyingine ya chama hicho kujivua gamba.
Ningetarajia kuona CCM kwa nafasi yake kama chama
tawala ikionyesha mfano kwa kuchukua hatua dhidi ya wanachama na
viongozi wasiotimiza wajibu wao, badala ya kutuonyesha sinema za bure za
kulalamikia watendaji wake kwenye mikutano ya hadhara.
Mathalan, malumbano yanayoendelea baina ya Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye na baadhi ya mawaziri kwa
kuwaita kuwa ni mzigo na kupendekeza wang’olewe ni sawa na kujikausha
maji ukiwa ndani ya bahari ukioga. Mbona ilikuwa ni rahisi kwa CCM
kumaliza suala hilo kwenye vikao vya ndani ambavyo mwenyekiti, Rais
Jakaya Kikwete ndiye aliyewateua mawaziri hao?
Kauli kama hizo za mawaziri mizigo, zingekuwa na mashiko kama
zingekuwa zinatolewa na vyama vya upinzani na CCM kuwasilikiza na
kuchukua uamuzi mgumu dhidi yao.
Pamoja na ujasiri wa kuchukua maamuzi magumu, kwa
upande wa Chadema, demokrasia pia ichukue mkondo wake, isijekuwa kweli
kama inavyodaiwa, kuwa kila anayejitokeza kuwania nafasi ya uenyekiti
anakutana na rungu zito la kuvuliwa vyeo au kutimuliwa. 0759292662