Dr. Slaa akubali kusogeza mbele ziara ya kutembelea majimbo nane ya mkoa wa Kigoma


MWANGWI wa uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema wa kumvua madaraka aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto  Kabwe na wenzake, mbali na kutikisa katika kanda sita kati ya kanda nane muhimu za chama hicho nchini, sasa umeanza kukubalika na Sekretarieti ya chama hicho Taifa.
 
Jana Kurugenzi ya Habari ya Chadema, ilituma ratiba ya ziara za Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, mikoani iliyoonesha amekubali ushauri wa kusogeza mbele ziara ya kutembelea majimbo nane ya Kigoma.
 
Awali Dk Slaa alitarajiwa kuanza ziara ya kuimarisha chama mkoani Kigoma kuanzia kesho lakini juzi Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kigoma, Jafari Kasisiko, alisema baada ya kutafakari kwa kina na kwa kutumia hekima na busara, walipendekeza ziara hiyo isogezwe mbele...
 
Sababu za mapendekezo hayo kwa mujibu wa Kasisiko, ni kutoa nafasi kwa uongozi wa Mkoa, kwenda kuwaelimisha wanachama kutii uamuzi wa Kamati Kuu wa kumvua madaraka Zitto na wenzake, hata kama uamuzi huo umewaudhi, lakini lengo ni kudhibiti vitisho vya kuvuruga amani katika ziara hiyo vilivyokuwa vimetolewa.
 
“Mkoa uliomba Taifa liahirishe na kusogeza mbele tarehe ya ziara hiyo muhimu kwa mkoa wetu, ili Mkoa kama ngazi ya chini ya Kanda na Taifa, uende katika majimbo hayo na kuwaelimisha wanachama na wapenzi wetu, kuhusu kuheshimu na kuwa na nidhamu na uamuzi utolewao na ngazi ya juu yetu, hata kama una maumivu.
"Maoni ya wengi mkoani na kwa viongozi wa Chama ni kuudhiwa na uamuzi wa Kamati Kuu ambao ni dhahiri ulilenga kummaliza Zitto kisiasa.
 
"Mkoa ulitishika na vitisho baada ya kupokea taarifa kutoka kwa baadhi ya viongozi wa majimbo ya Mkoa, kuwa hali ya usalama si nzuri kwa ujio wa kiongozi wetu Dk Slaa… endapo hali haitokuwa salama Mungu aepushie mbali,” alisema Kasisiko katika taarifa yake.
 
Dk Slaa ashaurika
Pamoja na Chadema kusisitiza kuwa ziara hiyo itakuwepo, lakini taarifa ya jana ya Kurugenzi ya Habari ya Chadema, ilieleza kuwa badala ya kuanza ziara mkoani Kigoma kama ilivyokuwa awali, sasa ataanza ziara ya siku 20 kuanzia leo lakini mkoani Shinyanga.
 
Bila kufafanua atakaa Shinyanga kwa siku ngapi, taarifa hiyo ilifafanua kwamba ziara hiyo itamfikisha Dk Slaa mpaka mkoani Kigoma, ingawa haikueleza lini atakwenda katika mkoa huo anakotoka Zitto na atakaa kwa siku ngapi.
 
“Siku ya Jumatano Desemba 4 mwaka huu (leo), Katibu Mkuu Dk Slaa atakuwa Wilaya ya Kahama, siku inayofuata Desemba 5, atakuwa Wilaya ya Kakonko, Jimbo la Buyungu na Desemba 6, atakuwa Jimbo la Muhambwe. Ratiba ya siku zinazofuata itaendelea kutolewa kwa vyombo vya habari,” ilieleza taarifa hiyo ya Kurugenzi ya Habari ya Chadema.