Alichokiandika Johnson Mbwambo mwaka 2012 na kilichomtokea Kagasheki 2013


TAFAKURI JADIDI: Kagasheki atauweza mfupa uliowashinda mawaziri wanne?
Makala ya Johnson Mbwambo katika gazeti la RAIA MWEMA, Toleo la 248, Julai 11, 2012
  Mbwambo 
 
KUNA Watanzania wameanza kusisimshwa na utendaji kazi wa Waziri Mpya wa Maliasili na Utalii, Hamis Kagasheki. Asili ya kusisimshwa kwao ni namna alivyoanza kazi mara baada ya kuteuliwa kuiongoza wizara hiyo badala ya Ezekiel Maige.


Siku chache tu baada ya kuingia ofisini, Waziri Kagasheki aliwashukia kwa kishindo na kuwasimamisha kazi maofisa wanaotuhumiwa kuhusika na kuuawa kwa faru wawili huko Serengeti.

Majuzi hapa Kagasheki alitema tena cheche nyingine alipowasimamisha maofisa 10 waandamizi katika wizara yake kupisha uchunguzi dhidi yao. Wakati akiwasimamisha maofisa hao, Waziri Kagasheki alitangaza kuwa sasa ameanza kazi rasmi kuisafisha wizara hiyo.

Hayo na mengine kadhaa ndio yanayowaaminisha baadhi ya Watanzania kwamba wizara sasa imepata kiongozi mahiri, na mchapakazi  kweli kweli.

Niseme mwanzoni kabisa kwamba mimi si mmoja wa hao wanaoamini kuwa wizara sasa itatulia kwa sababu ipo chini ya 



kamandoo mahiri aliyepania kupambana na ufisadi uliokithiri katika wizara hiyo.

Nijuavyo mimi, na nikizingatia rekodi za nyuma, hatua hizi za sasa za Kagasheki ni “nguvu za soda” tu; kwani hata mawaziri wengine wa wizara hiyo waliomtangulia walianza hivyo hivyo!

Wote waliotangulia walitamba bungeni wakati wakiwasilisha bajeti zao kwamba wataisafisha wizara hiyo, lakini hilo halikutokea, na waliishia kuhamishwa wizara au kuenguliwa kabisa uwaziri.

Nina hakika Kagasheki naye atatamba hivyo hivyo wakati atakapowasilisha bajeti yake, kwa mwaka wa fedha 2012/13, Jumatano ya Julai 11. Ni muda gani atadumu katika wizara hiyo, ni suala la muda tu jibu litafahamika.

Kitakachomkwaza Waziri Kagasheki, na ambacho ndicho kilichowakwaza mawaziri wenzake waliomtangulia, ni vigogo wenye ushawishi mkubwa nchini katika sekta ya utalii na misitu. Hao ndio waliosababisha kung’atuliwa kwa mawaziri waliomtangulia, na wa mwisho akiwa Ezekiel Maige.

Na kwa sababu vigogo hao bado wapo, na bado wana ushawishi mkubwa kwa watawala wetu, ni vigumu kwa Waziri Kagasheki kukomesha ufisadi katika wizara hiyo; hata kama atatimua maofisa wote wa ngazi za juu wa wizara hiyo na kuweka wapya! Ilimradi vigogo hao wenye ushawishi mkubwa bado wapo, itakuwa tu ni business as usual!

Uwepo wa mtandao huo wa vigogo wenye ushawishi mkubwa kwa watawala wetu umethibitishwa karibu na mawaziri wote waliopitia wizara hiyo katika miaka ya karibuni ya utawala wa Rais Kikwete; yaani kina   Anthony Diallo, Jumanne Maghembe, Ezekiel Maige, nikiwataja wachache.

Hebu tukumbushane ushuhuda wao tukianzia na Diallo. Huyu alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, mwaka 2006, alitangaza kwamba biashara haramu ya uuzaji magogo nje ya nchi ilikuwa ikifanywa na vigogo kadhaa wenye nguvu; huku baadhi yao wakiwa serikalini.

Waziri huyo alibainisha kuwa, makampuni mengi yaliyosajiliwa yanayofanya biashara haramu ya kuuza magogo nje ya nchi yanamilikiwa (kwa siri) na baadhi ya viongozi waandamizi serikalini kwa kushirikiana na vigogo kadhaa.

Waziri Diallo hakupata kuyataja majina ya viongozi hao, lakini baadaye aliondolewa katika wizara hiyo. Inaaminika kuondolewa kwake katika wizara hiyo kulikuwa na ‘mkono’ wa mmoja wa vigogo hao wenye ushawishi mkubwa kwa watawala wetu.

Ushuhuda mwingine wa uwepo wa vigogo hao wenye ushawishi mkubwa wanaokwamisha juhudi za kumaliza ufisadi katika wizara hiyo, ulitolewa na Waziri Maghembe.

Baada ya kukaa katika wizara hiyo kwa muda mfupi tu, Waziri Maghembe naye aliirudia kauli hiyo ya mwenzake kwamba wanaojihusisha na biashara hiyo haramu ya magogo nchini, ni vigogo wenye ushawishi mkubwa nchini.

Kwa hakika, Waziri Maghembe yeye alikwenda mbali zaidi kwa kuliambia bunge kwamba tayari alishamkabidhi Rais Kikwete orodha nzima ya vigogo hao. Mpaka leo majina yaliyomo kwenye orodha hiyo ya Waziri Maghembe yamebakia kuwa siri ya Ikulu!

Lakini ushuhuda wa hivi karibuni kabisa wa kuwepo kwa vigogo hao wenye ushawishi mkubwa wanaokwamisha vita dhidi ya ufisadi katika wizara hiyo ulitolewa na Ezekiel Maige mara baada ya kutemwa uwaziri.

Maige aliufahamisha umma kwamba vita dhidi ya ufisadi katika wizara hiyo inakwamishwa na vigogo hao, na kwamba kung’olewa kwake kuwa waziri wa wizara hiyo kunatokana na ushawishi wao; hasa baada ya kumuona ni kikwazo.

Maige alisema ya kuwa vigogo hao hawakufurahishwa na namna alivyolivalia njuga suala la utoroshaji wanyama hai nje ya nchi au ugawaji mzuri wa vitalu vya uwindaji, na hata udhibiti wa biashara haramu ya uuzaji magogo nje ya nchi.

Tofauti pekee kati ya Maige na wenzake wawili – Maghembe na Diallo, ni kwamba yeye aliweka mambo hadharani baada ya kuwa ametimuliwa uwaziri wakati wenzake walitoboa siri hiyo wakati bado wakiwa mawaziri.

Vyovyote vile; tulichojifunza kutoka kwa ushuhuda wa mawaziri wote watatu ni kwamba wanaokwamisha vita dhidi ya ufisadi katika wizara hiyo ni watu wenye nguvu kubwa nchini ambao mawaziri hawana ‘ubavu’ wa kuwagusa.

Na ndio maana nasema kwamba; ilimradi vigogo hao bado wapo, ilimradi mtandao wao bado upo, na ilimradi wanaendelea kukingiwa kifua na watawala wetu, Waziri Kagasheki na juhudi zake za sasa ataishia tu kule kule walikoishia wenzake waliomtangulia.

Lakini  tumwonee huruma zaidi Waziri Kagasheki kwa sababu adui yake sasa si vigogo hao tu; kwani ameongezeka adui wa pili katika biashara haramu ya kuuza magogo nje ya nchi na pembe za wanyama  - adui huyo mpya ni Wachina!

Tangu Serikali ya China ilipoweka sheria kali kulinda misitu ya China mwaka 1998, viwanda vya nchi hiyo vimekuwa vikikimbilia bara la Afrika kupata mahitaji yao makubwa ya mbao kwa njia haramu. Hivi sasa asilimia 60 ya magogo yanayovunwa nchini kwa njia za haramu huishia China!

Asasi ya Uingereza inayojishughulisha na uchunguzi wa biashara haramu za maliasili – Environmental Investigation Agency (EIA) imeeleza katika ripoti yake kwamba, Wachina wanajishughulisha na biashara haramu za pembe za ndovu, vifaru na pia magogo katika pwani ya Tanzania na Msumbiji; hususan maeneo ya Cabo Delgado na Nampula.

EIA, ambayo kwa miaka 10 imekuwa ikifuatilia kiuchunguzi ushiriki wa makampuni ya kichina katika biashara hizo haramu barani Afrika, inasema kwamba, maofisa wa China hutumia watu wa kati katika biashara hizo, na kwamba meli zao husafirisha kila mwaka shehena za magogo kupeleka China.

Lakini bila hata kurejea utafiti huo wa EIA, wengi wetu tunafahamu kuwa mara nyingi baadhi ya Wachina wanaokuja nchini kwa ajili ya miradi ya ujenzi pia hujihusisha na biashara haramu ya magogo na pembe za wanyama.

Na mara nyingi watawala wetu wanasita kuwanyooshea vidole au kuwatia mbaroni, kwa sababu ya kubweteshwa na ‘misaada’ na ‘mikopo laini’ ya Serikali ya China.

Na Wachina wanalijua hilo, na ndio maana hupendelea zaidi kujihusisha na biashara hizo ovu katika nchi za Afrika ambazo mifumo yake ya uongozi si imara zikiwemo DR Congo, Sudan na Zimbabwe.

Kwa hiyo, Waziri Kagasheki si tu kwamba atakwamishwa na vigogo hao wenye ushawishi mkubwa katika juhudi zake za kukomesha utoroshaji wanyama hai nje ya nchi, ugawaji kifisadi vitalu vya kuwindia wanyama au uuzaji haramu wa magogo nje ya nchi, lakini pia itabidi apambane na mafisadi wapya wanaochangia kuteketeza misitu yetu – Wachina!

Ni ugumu huu unaotufanya baadhi yetu tuwe na shaka kama kweli Waziri Kagasheki atauweza mfupa uliowashinda wizarani hapo kina Maghembe, Diallo na Maige.

Ni suala la muda tu tutajua kama naye zake zilikuwa ni nguvu za soda tu sawa na ilivyokuwa kwa mawaziri waliomtangulia!

Tafakari