
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert
Manumba amestaafu rasmi utumishi wa umma baada ya kufikia umri wa
kustaafu kisheria wa miaka 60.
Manumba
aliyeanza kulitumikia Jeshi la Polisi miaka ya 1970, nafasi yake
itashikwa kwa muda na Mkuu wa Ufuatiliaji na Tathmini (CID), Kamishna
Isaya Mungulu.
“Wakati
utaratibu wa uteuzi wa Mkurugenzi wa Upelelezi ukiendelea, Kamishna
Mungulu, atakaimu nafasi hiyo,” ilisema sehemu ya taarifa ya Polisi kwa
vyombo vya habari iliyotolewa jana na Msemaji wake, Advera Senso.
Akizungumzia
kustaafu huko, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema,
amemshukuru na kumpongeza Manumba kwa weledi na uaminifu mkubwa
aliouonyesha wakati wote alipokuwa mtumishi wa Jeshi la Polisi.
Amemtaka
aendelee kuwa msaada kwa jeshi hilo kwa kutoa ushirikiano wa namna
yoyote ile unaoweza kusaidia kupunguza uhalifu nchini akisema usalama
ni taaluma kama zilivyo nyingine.
Historia yake kikazi
Katika
utumishi wake, DCI Manumba amelitumikia jeshi hilo katika nyadhifa
mbalimbali zikiwamo katika Chumba cha Kupokea Mashtaka kati ya mwaka
1976 hadi 1977 na baadaye Mwendesha Mashtaka Wilaya ya Kibondo na
Kasulu mkoani Kigoma kati ya 1977 na 1984.
Alikuwa
Mkufunzi katika Chuo cha Polisi kilichopo Kurasini Dar es Salaam, kati
ya mwaka 1984 na 1987 kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya
ya Kipolisi ya Magomeni na Kinondoni. Manumba baadaye aliteuliwa kuwa
Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuanzia 1987 hadi 1993.
Kati
ya mwaka 1993 na 1995, alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha
kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa Mkufunzi Mkuu wa Chuo cha Polisi
Moshi kati ya 1995 na 1996.
Aliteuliwa
kuwa Mkuu wa Kitengo cha Kukabiliana na Uhalifu wa Kughushi Makao Makuu
ya Upelelezi mwaka 1996 na 1997 na baadaye kuwa Mkuu wa Kitengo cha
Usalama, Intelijensia na Kupambana na Biashara ya Dawa za Kulevya
kwenye Makao Makuu ya Upelelezi kuanzia 1997 hadi 2001.
Mwaka
2001 hadi 2006 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai na kuanzia mwaka 2006 hadi anastaafu, alikuwa
Mkurugenzi wa idara hiyo.
Mapema
Januari, jina la DCI Manumba lilitawala vyombo vya habari baada ya hali
yake kuwa mbaya na kulazwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU),
Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.
Januari 26 mwaka huu, alipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi katika Hospitali ya Milpark, Johannesburg.
Alirejea
nchini Aprili 23 baada ya miezi miwili na kusema ni mkono wa Mungu
uliomfanya apate nafuu kubwa baada ya juhudi kubwa za madaktari
kupigania uhai wake.