
Siku chache baada ya kumalizika kwa Mkutano wa 13 wa Bunge,
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Deo
Filikunjombe amesema kamati yake inashindwa kutekeleza majukumu yake
ipasavyo kutokana na kubanwa na Ofisi ya Spika.
Kauli
hiyo imekuja siku chache baada ya Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamisi
Kigangwala kuongoza harakati za kumng’oa Spika wa Bunge Anne Makinda
kwa madai kuwa anaongoza Bunge kwa upendeleo na hasa kwenye uendeshaji
wa kamati. Alikusanya saini za wabunge wapatao 30 ili waunge mkono hoja
yake, ambayo kwa sasa inashughulikiwa na Kamati ya Haki, Kinga na
Madaraka ya Bunge.
Filikunjombe
ambaye pia ni Mbunge wa Ludewa (CCM), alisema hayo jana wakati wa
ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa PAC na Kamati ya
Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC), yaliyohudhuriwa pia na Ndugai pamoja
na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh.
Alisema
mara nyingi kamati hiyo inapozihoji idara mbalimbali, Spika Makinda au
Naibu wake, Job Ndugai wamekuwa wakiwapigia simu na kuwataka kutoruhusu
vyombo vya habari kusikiliza majadiliano hayo, kitendo alichosema kuwa
kinazorotesha uwajibikaji.
“Mara
nyingi tumekuwa tukipokea simu kutoka kwao zinazolalamikia utendaji wa
kamati hii,” alisema na kuongeza: “Hatua hiyo inatokana na kamati (PAC)
kuwa na tabia ya kuruhusu vyombo vya habari kuingia katika vikao vyetu
wakati tunapokuwa tunahoji watendaji wa idara mbalimbali. Wamekuwa
wakitupigia simu na kututaka tusifanye hivyo.”
Ndugai
alisema kanuni za Bunge zinaruhusu vyombo vya habari kushiriki katika
vikao vya kamati za Bunge lakini wanaandaa utaratibu wa ushiriki wao.
“Kuanzia
sasa tunajaribu kuangalia namna ya kuweka utaratibu ili kuvisaidia
vyombo vya habari kupata taarifa za matumizi ya fedha za umma bila ya
kuathiri utendaji wa kamati,” alisema.
Filikunjombe
alipendekeza kubadilishwa kwa kanuni ili vikao vya PAC na LAAC virushwe
moja kwa moja katika televisheni kama ilivyo mikutano ya Bunge ili kama
kuna mtu anasema uongo wananchi wamwone.
Alisema
hali hiyo itasaidia watendaji kuongeza uwajibikaji na uwazi katika
matumizi ya fedha za umma… “Inashangaza… maana tukiwaita watendaji
kujieleza mbele ya kamati juu ya matumizi ya fedha tunapigiwa simu na
Spika Makinda au Naibu wake, hii inaondoa dhana nzima ya uwajibikaji,”
alisema.
Alisisitiza
kuwa idara hizo huwa zinaomba fedha za umma bila kificho kwa nia ya
kuzitumia kwa mambo ya msingi lakini ameshangazwa na hofu ya viongozi
kuhojiwa wakati vyombo vya habari vikiwapo.
Alisema umefika wakati kwa Ofisi ya Spika kuziamini kamati na kuziacha zifanye kazi zake kwa umakini ili kuwa na uwajibikaji.
“Ni
vizuri kamati hizi mbili zikaachwa zifanye kazi zake kwa sababu zina
umuhimu mkubwa katika usimamizi wa fedha za umma,” alisema Filikunjombe.
CAG aililia POAC
Kwa upande wake, Utouh alisema kuna haja ya Spika Makinda kuunda kamati nyingine ili ifanye kazi ya kukagua mashirika ya umma.
Bunge
lilifanya mabadiliko ya muundo wa kamati zake mwaka huu na PAC
iliongezewa kazi ya kukagua hesabu za mashirika ya umma baada ya
kuvunjwa kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).
“Kamati
ya POAC ilikuwa na umuhimu wake. Umefika wakati Bunge likaona umuhimu
wa kazi zilizokuwa zikifanywa na kamati hiyo ya kukagua mashirikia
badala ya kuiachia PAC mzigo mkubwa,” alisema Utouh.
Mwenyekiti
wa LAAC, Rajab Mbaruku Mohamed alisema katika kipindi cha miaka miwili,
Ofisi ya Bunge imeshindwa kuwapa fedha za kuwawezesha kukagua miradi ya
maendeleo.
“Kamati
zimechoka kuwa washauri, sasa tunataka kupewa meno ili tuweze hata
kufuatana na polisi tunapokwenda kufanya ukaguzi,” alisema.