Kwanza,
niseme hapa wazi kwamba, ni mwendawazimu tu ama mtu asiyeelewa
mahusiano ya Mhe. Deo Filikunjombe (Mb.) na Mhe. Spika Anne Makinda
(Mb.) ama na Mhe. Kangi Lugora (Mb.), atakayepata tabu kuelewa kwa nini
watu hawa wamenishambulia kwenye magazeti na mitandao ya kijamii. Deo
Filikunjombe ni 'mtoto wa mama' Anne Makinda!
Pili, niseme pia
kwamba watu wa aina hii hawakustahili kujibiwa lakini kwa ushauri wa
wabunge wengi wanaoniunga mkono nimeamua niwajibu. Hawa wabunge wenye
kuja na nyoka wa dhahabu bungeni na kujigamba wao ni majasiri kwa kuwa
'walisaini karatasi ya hoja ya kumng'oa Waziri Mkuu na baada ya
kushughulikiwa na wabunge wenzao wa CCM walianza kulia lia kwa
Mwenyekiti wa Chama kuwa wasamehewe kwa kuwa waliasi chama kwa sababu
wamebanwa sana majimboni mwao na wanaCCM wenzao na pia na wapinzani',
kwa hakika hawakustahili majibu toka kwangu. Tabia za ukinyonga namna
hii ni ujasiri, udandiaji hoja ama kutokujua wanalofanya ndani ya Bunge?
Hawa wabunge wanaopiga makelele kutetea CHC kumbe wamelambishwa mzigo.
Hawa wabunge wanaojidai wao ni wazalendo wanaojipambanua kwa kupinga
ufisadi wa mawaziri kumbe wenyewe wanachukua hela za mashirika
wanayoyakagua. Huu ni uzalendo ama kudanganya wananchi wasiojua ukweli
na uhalisia wa sura za watu hawa?
Tatu, naomba nitumie fursa
hii kusema kuwa hoja yangu, inayoungwa na wabunge wengi inajikita zaidi
kwenye kumuwajibisha Spika wa Bunge kwa kukiuka masharti ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 63 (2), ibara ya 100, kwa
kutuzuia wabunge tusiiingize jedwali la marekebisho wakati wa kutunga
sheria ya fedha kwa kututaka tuyapeleke mbele ya Kamati ya Mhe. Andrew
Chenge (Mb.) kinyume na Kanuni za Bunge, na hivyo kusababisha vifungu
vyenye mambo ya hovyo kama ya 'kodi ya simcard' vipite bila kupingwa na
wabunge. Wachunguzi wa mambo kasomeni hansard za Bunge za kuanzia tare
26 Juni 2013 mje mkanushe kama kuna mbunge aliruhusiwa kuleta Bungeni
jedwali la marekebisho. Mimi nilikuwa na jedwali lenye mapendekezo ya
marekebisho 19, Mnyika vile vile, Wenje, Sakaya, Soni, Mangungu na
wengineo - sote sisi tulikataliwa kuleta majedwali yetu Bungeni.
Kasomeni pia na nyie Kanuni zinasemaje kuhusu namna ya kupitisha Sheria
wakati wa muswada kusomwa kwa mara ya pili Bungeni?!
Binafsi,
nimeishawasilisha hoja binafsi zifuatazo, ya madini Nzega (nimeipeleka
Bungeni zaidi ya mara 8 na sikupewa nafasi), ya kuzuia ugawaji vitalu
vipya vya gesi (mara 3), ya madawa ya kulevya (mara 2), ya kuzuia
uingizaji wa Genetically Modified Organisms, ya kufanya marekebisho ya
mifuko ya hifadhi ya jamii (mara 2), ya kuanzisha mfuko wa kulinda bei
za wakulima (price stabilisation fund), na pia muswada binafsi
nikishirikiana na wabunge wengine 8 (kuanzisha parliamentary budget
office). Waluizeni wabunge wenu wameishawasilisha hoja zao mara ngapi
na wameruhusiwa mara ngapi?
Hoja yangu inajikita kwenye
kumwondoa Spika madarakani kwa kushindwa kusimamia Sheria ya Bunge ya
mwaka 2008, kushindwa kuzilinda Kanuni za Bunge; mfano anapozuia hoja
binafsi na miswada binafsi ya wabunge isiingizwe bungeni kwa kisingizio
hakuna muda ilhali sababu kubwa ni kuwa hana bajeti na anafanya kazi
kinyume na utaratibu wa Sheria ya Bunge ya mwaka 2008 inayotaka Bunge
liwe na mfuko wake ili lisiendeshwe na namna serikali inavyotaka. Bunge
linapokuwa tegemezi kwa serikali maana yake ile 'doctrine ya separation
of power' inakuwa majaribuni. 'Mfuko wa Bunge' ambao ungemwezesha
kupanga shughuli za bunge kwa kadri anavyoona inafaa badala ya
kutegemea apate pesa kutoka serikalini ambapo humpa za kutosha
kushughulikia shughuli za serikali tu na hivyo kuwanyima wabunge haki
ya uwakilishi haupo hadi leo wakati unapaswa kuwepo kwa mujibu wa
sheria niliyoitaja hapo juu.
Mfano mwingine ni pale
anavyotumia Kanuni ya 48, inayohusu mambo ya dharura, vibaya na hivyo
kukataa mijadala yote ya dharura - mfano pale boti ya MV Skagit
ilipozama kandoni mwa kisiwa cha Chumbe na yeye Spika akaona hili si
jambo la dharura. Watu wanakufa, wabunge wanataka tusitishe shughuli za
Bunge tujadili jambo la dharura, yeye anadai hilo si jambo la dharura!
Kuna mambo mengi zaidi ya haya machache niliyoyataja hapa. Kuna la
kuteua Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Mhe Andrew Chenge (Mb.) kinyume
na Kanuni na taratibu za Bunge. Kesho tunaweza kufanya mkutano na
waandishi wa habari na hivyo kuweka hadharani hoja yenyewe na kujibu
maswali kwa waandishi wa habari ili suala hili lieleweke vizuri.
Nne, hoja hii haizungumzii posho hata kidogo, ni watu wa aina ya hawa
wawili tu wanaoweza kupata tabu kuelewa muktadha wa hoja nzito kama
hii. Na hawa wanapata upofu huu aidha kwa kuwa wana 'maslahi binafsi'
ama uelewa mdogo wa Kanuni za Bunge. Ningewashauri waje wahudhurie
kikao tutakachofanya kesho kujadili namna tutakavyoipitisha hoja hii na
kufanikisha kumwondoa madarakani Spika Makinda kwa kukiuka Kanuni mara
nyingi zaidi katika historia kuliko maspika wote waliomtangulia!
Tano na mwisho, wabunge hawa 'waoga na wanafiki' wakome kuvamia mambo
wasiyoyajua na wafahamu mimi huwa sidandii hoja za watu kama wao. Aina
ya siasa zangu si kama za kwao, za kukurupuka na kusema maneno mepesi
mepesi ilimradi tu waonekane wanapinga serikali kwenye kila kitu.
Ahsanteni,
HK.