Mheshimiwa Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo Pinda, Waziri Mkuu;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Mheshimiwa Freeman Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni;
Waheshimiwa Wabunge;
Mabibi na Mabwana;
Nakushukuru sana Mheshimiwa Spika kwa kukubali ombi langu na kutenga
muda wenu ili niweze kuzungumza na Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuhusu
masuala muhimu kwa uhai, ustawi na maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Mheshimiwa Spika;
Nimeambiwa kuwa taarifa ilipotolewa kuwa ninaomba kuja kuzungumza na
Waheshimiwa Wabunge, kumekuwepo na dhana mbalimbali. Wapo waliodhani
kuwa nakuja kuzungumzia mchakato wa kuunda Katiba mpya na hasa matukio
ya wiki chache zilizopita. Wapo waliodhani nakuja kuzungumzia
“Operesheni Tokomeza”. Tena wapo waliokwenda mbali na kufikiria kuwa
nakuja kuwakaripia Waheshimiwa Wabunge waliotoa maoni yao kuelezea
kasoro zilizojitokeza katika utekelezaji wa Operesheni hii muhimu. Na
wapo pia waliodhani ninakuja kuzungumzia ushiriki wa majeshi yetu ya
Tanzania katika Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa nchini Kongo.
Mheshimiwa Spika;
Hayo si makusudio yangu. Kinachonileta mbele ya Bunge lako Tukufu ni
kuzungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki na mustakabali wa Tanzania
katika Jumuiya hiyo. Lakini, kwa sababu ya umuhimu wa masuala hayo
niliyoyataja na rai niliyopewa kuwa niyasemee japo kidogo. Nimeona ni
vyema nifanye hivyo.
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu mchakato wa Katiba
mpya, napenda kusema kuwa tumefikia hatua nzuri katika utekelezaji
wake. Kama mjuavyo Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekamilisha, kwa
mafanikio, hatua ya mwanzo ya kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu Katiba
wanayoitaka. Pia walishatoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba na kukamilisha
mchakato wa Mabaraza ya Katiba. Kinachosubiriwa kwa hamu na sisi wote,
ni Rasimu ya Pili ya Katiba ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe
15 Desemba 2013 au kabla ya hapo.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande
wa Bunge lako Tukufu, tunategemea kupata mambo mawili kutoka kwenu
yatakayowezesha mchakato kutekelezwa vizuri katika hatua zinazofuata.
Jambo la kwanza ni kutungwa kwa Sheria ya Kura ya Maoni na pili
kufanyika kwa marekebisho ya nyongeza ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
kuhusu Bunge Maalum ili kuboresha utekelezaji wake. Baada ya Bunge
kukamilisha kazi yake hiyo itafuatia uteuzi wa Wajumbe wa Bunge Maalum
ili kazi ya kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba ifanyike na kutupatia
Rasimu ya Mwisho. Rasimu ambayo ikikubaliwa na wananchi katika Kura ya
Maoni itakayofanyika wakati wo wote mwakani, tutakuwa tumepata Katiba
Mpya. Hivi sasa katika Serikali tunaendelea kufanya tafakuri na
tunachukua hatua za kuwezesha Bunge Maalum na Kura ya Maoni kufanyika
kwa mafanikio.
Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika;
Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuwa
sikukasirishwa na maoni yao kuhusu madai ya kuwepo kasoro katika
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Shabaha ya Operesheni hii ni kuokoa
maliasili za misitu na wanyamapori dhidi ya uvunaji haramu ambao
umefikia kiwango kinachotishia kutoweka kwa raslimali hizo. Kwa kweli
hali inatisha. Miti inakwisha na ndovu na faru wanaangamia.
Mheshimiwa Spika;
Wakati, tunapata Uhuru Tanzania ilikuwa na ndovu waliokadiriwa kuwa
takribani 350,000. Lakini, kwa sababu ya ujangili uliokithiri katika
miaka ya 1970 na 1980 ilipofika mwaka1989 kulikuwa na ndovu wapatao
55,000 tu. Ilipofikia hali hiyo Serikali ikaanzisha Operesheni Uhai
iliyohusisha Jeshi la Ulinzi na kuongozwa na Meja Jenerali John Walden
(ambaye sasa ni marehemu) kuendesha mapambano dhidi ya majangili.
Kutokana na hatua hiyo na uamuzi wa Shirika linalosimamia biashara ya
wanyama walioko kwenye hatari ya kutoweka (CITES) kupiga marufuku
biashara ya pembe za ndovu duniani, idadi ya ndovu nchini iliongezeka na
kufikia 110,000 mwaka 2009.
Tumewaomba Fankfurt Zoological
Society ambao ni wabia wetu katika uhifadhi wa wanyama pori kwa miaka
mingi wafanye sensa maalum ya ndovu katika Hifadhi ya Selous na kote
nchini ili tujue hali halisi ikoje. Kazi hiyo inaendelea hivi sasa.
Mheshimiwa Spika;
Baada ya mwaka 2009 kumezuka wimbi jipya, tena la nguvu kubwa, la kuua
ndovu na faru nchini na kwingineko katika Bara la Afrika ambako wanyama
hao wapo. Idadi kubwa ya meno ya ndovu yaliyokamatwa na yanaoendelea
kukamatwa nchini na kwingineko duniani inathibitisha ukweli huo. Kwa
mfano, kati ya mwaka 2010 na Septemba, 2013, hapa nchini, kwa jitihada
zetu vipande 3,899 vya pembe za ndovu vyenye uzito wa kilo 11,212 na
vipande 22 vya pembe za ndovu zilizochakatwa zenye uzito wa kilo
3,978vilikamatwa. Aidha, katika kipindi hicho vipande 4,692 vya pembe za
ndovu vilivyotokea Tanzania vyenye uzito wa kilo 17,797vilikamatwa nje
ya nchi.
Mheshimiwa Spika;
Kama nilivyokwisha sema hapo
awali matatizo ya kuuawa kwa wingi kwa ndovu na faru lipo pia katika
nchi nyingine Afrika zenye wanyama hao. Nchi za Gabon, Kenya, Afrika ya
Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Uganda, Zimbabwe, Zambia na
nyinginezo nazo zinakabiliwa na matatizo kama yetu. Tatizo limekuwa
kubwa kiasi cha kuifanya Jumuiya ya Kimataifa kushtuka na kuamua
kuingilia kati kwa namna mbili. Kwanza kuunga mkono juhudi za uhifadhi
wa ndovu na faru katika nchi zenye wanyama hao. Na, pili, kuchukua hatua
thabiti kudhibiti biashara ya meno ya ndovu duniani. Ni ukweli ulio
wazi kuwa kama hakutakuwepo na wanunuzi wa meno ya ndovu na faru hakuna
ndovu au faru atakayeuawa.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana na ukweli
ulivyo uamuzi wetu wa kuendesha Operesheni Tokomeza ni sahihi kabisa.
Manufaa yaliyopatikana baada ya Operesheni Uhai ya mwaka 1989 yanatupa
imani kuwa na safari hii pia tutafanikiwa. Tusipochukua hatua kama hii
sasa ni sawa na kuwapa kibali majangili waendelee kumaliza ndovu na faru
nchini. Hakika wanyama hao watakwisha. Itakuwa ni aibu kubwa kwetu na
historia itatuhukumu vibaya.
Mheshimiwa Spika;
Tumeyasikia
maelezo ya Wabunge kuhusu kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza. Nawaahidi kuwa tutayafanyia kazi.
Serikali imeahirisha kwa muda Operesheni hii ili kujipa muda wa
kurekebisha kasoro hizo na kujipanga upya. Watendaji wasiokuwa waadilifu
na wale wasiokuwa waaminifu wataondolewa. Halikadhalika, kasoro za
kimfumo nazo zitasahihishwa ili tutakapoanza upya Operesheni itekelezwe
kwa mafanikio yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika;
Miongoni
mwa mambo yaliyozungumzwa kwa uchungu ni ukamataji wa mifugo iliyokutwa
kwenye mapori ya hifadhi za wanyama na vitendo vibaya walivyofanyiwa
wenye mifugo na mifugo yenyewe. Narudia kusisitiza kuwa taarifa zote
hizo zitafanyiwa kazi na waliohusika watachukuliwa hatua zipasazo.
Pamoja na hayo, napenda kuwakumbusha ninyi watunga sheria wetu kuwa
sheria ya hifadhi za wanyamapori hairuhusu mifugo kuchungwa katika
maeneo ya hifadhi.
Naomba tuwakumbushe wananchi tunaowaongoza
wajiepushe na kufanya hivyo. Ni uvunjifu wa Sheria za nchi. Naomba pia,
wananchi waelimishwe ili wajue kuwa wakifanya hivyo na kukutwa katika
maeneo hayo na mifugo yao kuna adhabu iliyotamkwa kwenye sheria. Hivyo
tusiwalaumu wala kuwaona maafisa wanyamapori kuwa ni watu wabaya.
Wanatekeleza Sheria iliyotungwa na Bunge hili. Pale wanapotenda visivyo
tuseme, watawajibishwa ipasavyo.
Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo
Mheshimiwa Spika;
Mapema mwaka huu (2013) Umoja wa Mataifa uliomba nchi yetu ichangie
kikosi kimoja cha wanajeshi katika Brigedi Maalum iliyoundwa na Umoja
huo kuongeza nguvu ya kudhibiti waasi Mashariki ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo. Lengo la msingi ni kuiwezesha nchi hiyo kupata
amani ya kudumu ambayo imekosekana kwa muda mrefu kutokana na kuibuka
kwa uasi mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika;
Tulikubali, kwani
hata kabla ya kuombwa na Umoja wa Mataifa tulishakubali maombi kama
hayo yaliyotolewa kwenye Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu. Ni miezi saba
(tangu Aprili) sasa tangu wanajeshi wetu waende Kongo na wamekuwa
wanatekeleza majukumu yao vizuri tena kwa weledi na nidhamu ya hali ya
juu. Sifa hiyo kwa wanajeshi wetu imekuwa inatolewa na viongozi wa juu
wa Umoja wa Mataifa, viongozi wa juu wa Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo
(MONUSCO) na viongozi wa juu wa Serikali ya Kongo.
Mheshimiwa Spika;
Majeshi ya Umoja wa Mataifa hupewa majukumu na mamlaka ya namna mbili.
Yapo yanayopewa jukumu la kulinda amani tu. Wanajeshi wake huwa hawapewi
majukumu ya kimapigano na hata pale wanaposhambuliwa wanatakiwa
kujihami tu. Kwa kawaida majeshi yenye jukumu hili hupelekwa mahali
ambapo kumekuwepo na makubaliano ya kuacha mapigano. Wanapelekwa
kusaidia kuona Mkataba unatekelezwa ipasavyo.
Aina ya pili ni
ile ya majeshi yanayopelekwa mahali ambapo hakuna amani hivyo wanapewa
jukumu la kuchukua hatua za kufanya amani ipatikane. Majeshi haya hupewa
mamlaka ya kutumia nguvu ya kijeshi dhidi ya wanaosababisha amani
ikosekane kama ni lazima kufanya hivyo. Maana yake ni kwamba wanayo
ruhusa kuingia katika mapigano dhidi ya watu au vikundi vinavyovuruga
amani. Tofauti na wenzao wa kundi la kwanza, wanajeshi wa kundi la pili
wako kwenye hatari zaidi ya kupoteza maisha au kujeruhiwa kuliko wenzao
ingawaje wapo wengi nao wameuawa na kujeruhiwa.
Mheshimiwa Spika;
Wanajeshi wetu wamekwenda Kongo chini ya utaratibu huu wa pili ambao
unahusu kuingia kwenye mapigano dhidi ya waasi kama hapana budi kufanya
hivyo. Wametekeleza majukumu yao vyema na kwa ujasiri mkubwa na weledi
wa hali ya juu. Bahati mbaya tumepoteza vijana wetu watatu shupavu.
Daima tutawakumbuka na tutawaenzi ipasavyo mashujaa wetu hawa. Tuzidi
kuwaombea kwa Mola awape mapumziko mema. Ameen.
Wakati huo huo,
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Rais Joseph
Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa mafanikio ya kihistoria
waliyoyapata hivi majuzi dhidi ya waasi wa M23. Tunamtakia yeye na
wananchi wa Kongo kila la heri katika kazi ngumu iliyo mbele yao ya
kujenga upya eneo hilo na kujenga mahusiano mapya miongoni mwa watu wa
Kongo. Pia nawapongeza sana wanajeshi wa Brigedi Maalum ya Umoja wa
Mataifa kwa kazi nzuri waliyoifanya iliyowezesha mafanikio kupatikana.
Wanajeshi hao ni kutoka Afrika Kusini, Tanzania na Malawi wanaoongozwa
na Brigedia Jenerali James Aloisi Mwakibolwa wa JWTZ.
Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika;
Kama nilivyosema awali, haya mambo matatu siyo hasa makusudio yangu
nilipoomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge wetu. Nimeyachomekea
tu kwa sababu ya umuhimu wake katika jamii kwa wakati tulio nao. Jambo
lililonileta hapa leo ni kuzungumzia hali ilivyo sasa katika Jumuiya ya
Afrika Mashariki na nafasi ya Tanzania katika Jumuiya hiyo. Nimeona
nifanye hivyo kutokana na maswali mengi ambayo Watanzania wanajiuliza
kufuatia matukio ya hivi karibuni ya viongozi wa nchi tatu wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani Uganda, Rwanda na Kenya kukutana bila
ya ushiriki wa viongozi wa Tanzania na Burundi. Viongozi wenzangu hao
wamefanya mikutano mitatu yaani: tarehe 24-25 Juni, 2013 mjini Entebbe,
Uganda; tarehe 28 Agosti, 2013 mjini Mombasa, Kenya; na tarehe 28
Oktoba, 2013 mjini Kigali, Rwanda.
Mheshimiwa Spika;
Naomba
kwanza niweke wazi jambo moja, kwamba nchi mbili wanachama au zaidi
hazikatazwi kuwa na makubaliano ya ushirikiano katika kufanya mambo
mbalimbali. Hata sisi Tanzania tunao ushirikiano wa namna hiyo na nchi
zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lakini, nchi wanachama
zinatakiwa kufanya hivyo kwa yale mambo ambayo hayako kwenye shughuli za
Jumuiya kwa maana kwamba hayamo katika Mkataba au Itifaki au hakuna
uamuzi wa msingi uliofanywa na vikao au taasisi za Jumuiya
kuyashughulikia. Pia, tunaweza kufanya hivyo kwa mambo ambayo
yalishaamuliwa na Jumuiya yatekelezwe na ruhusa imetolewa kwa nchi yo
yote iliyokuwa tayari kutekeleza ama peke yake au kwa kushirikiana na
nchi nyingine.
Mheshimiwa Spika;
Kwa mujibu wa matamko ya
pamoja (Communique) yaliyotolewa baada ya mikutano hiyo, kuna mambo
yapatayomanane ya msingi yaliyoamuliwa kufanywa na nchi hizo kwa lengo
la kuendeleza utengamano wa nchi hizo wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Mambo hayo ni haya yafuatayo:
(1) Kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala, Kigali na Bujumbura.
(2) Ujenzi wa Bomba la Mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini.
(3) Kujenga Kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda.
(4) Kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutekeleza vipengele vyote;
(5) Kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki na kwamba itaundwa Kamati ya kuandaa rasimu ya Katiba ya Shirikisho.
(6) Kuharakisha uanzishwaji wa Visa ya pamoja ya Utalii ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki (Single East African Community Tourist Visa);
(7) Kuandaa utaratibu wa kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria katika nchi zao; na
(8) Kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika;
Ni dhahiri kwamba orodha hiyo imechanganya mambo yale ambayo ni ya
Jumuiya na yale yasiyo ya Jumuiya. Kwa mfano, mambo manne kati ya hayo
manane hayamo kwenye masharti ya kutokufanyika bila ya kuihusisha au
kupata ridhaa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Jambo la kwanza ni
uzalishaji na usambazaji wa umeme. Ni kweli kwamba tunao mkakati wa kuwa
na akiba ya pamoja ya nguvu ya umeme (East African Power Pool). Hata
hivyo, bado jukumu la kuzalisha na kusambaza umeme huo limeachiwa nchi
wanachama zenyewe kuamua. Lakini, hivi ndugu zetu hawa wanao muhali
kuishirikisha Tanzania katika mpango ambao kimsingi umebuniwa na Jumuiya
ya Afrika Mashariki ambayo sote ni wanachama?
Jambo la pili,
ni ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda. Hili si suala
la Jumuiya bali la nchi ya Uganda kuamua yenyewe peke yake au kwa
kushirikiana na wadau wengine. Rais Yoweri Museveni alituarifu mpango
huo na sote tuliupokea kwa furaha kwamba sasa tutapata mafuta karibu na
nyumbani. Alitualika kushiriki katika ujenzi wake sijui sasa amebadili
mawazo kwamba Tanzania siyo muhimu.
Mheshimiwa Spika;
Jambo
la tatu ni ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya hadi Sudani ya Kusini
na Uganda. Hili si jambo linalobanwa na masharti ya Jumuiya. Ni juu ya
nchi hizi tatu kuamua kufanya ili kuwezesha mafuta yao kufika kwenye
masoko. Hata hivyo, nimeambiwa kuwa Jumuiya imeshazungumzia bomba la
mafuta kutoka Eldoret hadi Uganda, Rwanda na Burundi kuwa nalo lifike
Tanzania kupitia upande wa Kaskazini Magharibi mwa Tanzania. Inaelekea
mpango huo sasa haupo maana hatujausikia kutajwa katika ujenzi wa bomba
hilo.
Mheshimiwa Spika;
Jambo la nne ni ujenzi wa reli ya
kisasa kutoka Mombasa – Kampala – Kigali – Bujumbura. Hili nalo hatuna
tatizo nalo. Si mradi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni jambo lililo
chini ya mamlaka ya nchi wanachama husika. Hata hivyo, ni vyema kutambua
ujenzi wa miundombinu ya reli, barabara na usafiri wa anga na majini
kuunganisha nchi za Afrika Mashariki ni miongoni mwa mambo ya kipaumbele
cha juu yanayoshughulikiwa na Jumuiya yetu. Jumuiya hutengeneza
mikakati ya pamoja na ndiyo maana tuna East African Railway Masterplan,
tuna East African Road Network, na tuna Lake Victoria Development
Programme kwa ziwa Victoria.
Kwa ajili hiyo, nilitegemea kuwa reli
ya kutoka Mombasa hadi Kigali na Juba ingekuwa na tawi linalounganisha
reli hiyo na reli ya Tanzania kama ilivyo reli ya Moshi – Voi – Taveta
aliyotuachia mkoloni. Tulitegemea hivyo kwa minajili ya kuunganisha soko
la Afrika Mashariki ambapo naamini Tanzania ni mdau muhimu. Lakini
inaelekea kwa maoni ya wenzetu hivyo sivyo.
Mheshimiwa Spika;
Lazima nikiri kuwa inashangaza na tunayo kila sababu ya kuuliza kwa nini
wenzetu wameamua kufanya hivi. Kumetokea nini toka tukutane pale Arusha
Aprili 28, 2013 na Juni 24, 2013 walipokutana kuamua kufanya mambo ya
kujenga na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kubaguana,
Haijawahi kuwa hivi kabla.
Mheshimiwa Spika;
Katika mambo
manne yaliyosalia ambayo yaliamuliwa na kuwekewa utaratibu wake wa
utekelezaji na Jumuiya ya Afrika Mashariki mawili hatuna maneno nayo.
Mambo hayo ni matumizi ya vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria
na Visa ya Pamoja ya Utalii kwani tuliamua kwa pamoja kuwa nchi
wanachama zilizokuwa tayari waanze. Lakini, kwa upande wa kuanzishwa kwa
Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory) na
Shirikisho la Afrika Mashariki tunadhani wenzetu wamekiuka uamuzi wetu
wa pamoja.
Mheshimiwa Spika;
Katika Mkutano Maalum wa 11 wa
Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe 28 Aprili, 2012 Jijini
Arusha, tulipokea na kuridhia mapendekezo ya kuanzisha Himaya Moja ya
Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory). Kwa mujibu wa mapendekezo
hayo kila nchi mwanachama itasimamia shughuli zake za kiforodha na
kukusanya mapato yake kama ilivyo sasa. Hata hivyo, kwa bidhaa
zinazopitia nchi moja kwenda nchi nyingine mwanachama, ukaguzi na
ukusanyaji wa mapato utafanyika katika kituo cha kwanza bidhaa hizo
zinapoingilia. Mapato hayo yatawasilishwa kwa nchi husika baada ya
kuthibitisha kuwa bidhaa zilivuka mpaka.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana na uamuzi huo, Wakuu wa Nchi waliagiza Baraza la Mawaziri
kuunda Kikosi Kazi cha kujadiliana na kuandaa utaratibu wa utekelezaji
wa mfumo huo. Taarifa ya kikosi kazi inatakiwa kutolewa katika Mkutano
wa 15 wa Wakuu wa Nchi utakaofanyika Kampala, Uganda tarehe 30 Novemba,
2013. Iweje leo nchi tatu wanachama ziamue peke yao kuanza kutekeleza?
Wanatekeleza nini na kwa nini wafanye hivyo?
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki hadithi yake inafanana
na hii ya Himaya ya Forodha. Katika Mkutano wa 14 wa Wakuu wa Nchi
wanachama uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2012, Nairobi, tulipokea
taarifa ya hatua iliyofikiwa kuhusu mchakato wa kutaka kuanzishwa kwa
Shirikisho. Mkutano huo uliagiza nchi wanachama kujadiliana zaidi kuhusu
mpango kazi wa kufikia Shirikisho la Kisiasa na mpango wa kutekeleza
mapendekezo mengine yaliyotolewa na Timu ya Wataalamu. Inategemewa kuwa
Baraza la Mawaziri litawasilisha mapendekezo ya majadiliano hayo katika
Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi mwezi Novemba, 2013. Iweje leo wenzetu
hawa waamue kuanzisha mchakato wao wa kuharakisha Shirikisho la Afrika
Mashariki.
Mheshimiwa Spika;
Kwa kweli huwa najiuliza
maswali mengi na kukosa majibu kuhusu nini kinachoendelea kufanywa na
viongozi wenzangu watatu na kwa nini! Nakosa majibu ya uhakika. Je
wenzetu wamekosa imani na Jumuiya ya Afrika Mashariki na je wanataka
kuunda yao? Je wanaichukia nchi yetu na hivyo wameamua kutufanyia
vitimbi tutoke! Au sijui wanachuki na mimi! Napenda kuwahakikishia
Waheshimiwa Wabunge kuwa hatuna mpango wa kutoka (kama vijana wasemavyo
hatoki mtu hapa). Tupo na tutaendelea kuwepo!
Mheshimiwa Spika;
Tanzania haijafanya jambo lo lote baya dhidi ya Jumuiya au nchi yo yote
mwanachama. Na ukweli ni kwamba ni mwanachama mvumilivu, mtiifu na
mwaminifu kwa Jumuiya. Tunatimiza ipasavyo wajibu wetu kwa Jumuiya na
kushiriki kwa ukamilifu katika ujenzi wake na utengamano ndani ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sabahu ya wenzetu watatu kuamua kufanya
mambo yahusuyo Jumuiya yetu peke yao kwa kweli haieleweki.
Mheshimiwa Spika;
Tunasikia eti kuwa baadhi yao walipoulizwa kwa nini wengine hatupo
wakasema kuwa wao wametangulia na sisi tutakapokuwa tayari tutajiunga.
Yaani wana Umoja wa Waliokuwa Tayari (Coalition of the Willing). Hivi ni
nani hayuko tayari (who is not willing?) Haiwezekani watu waitane
wenyewe bila ya kutualika halafu wadai kuwa wao ndiyo wako tayari na
kujenga dhana kuwa sisi wasiotualika ndiyo ambao hatuko tayari. Madai
hayo hayana ukweli. Ni vyema waseme ukweli. Kama walitualika tukakataa
ndiyo wanaweza kusema hayo.
Mheshimiwa Spika;
Kumekuwepo
na madai kutoka kwa baadhi ya wenzetu, eti kwamba Tanzania haina moyo
wala dhamira ya dhati ya kuendeleza utengamano wa Afrika Mashariki. Kwa
sababu hiyo inasemekana eti nchi yetu imekuwa kikwazo kwa maendeleo ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba Tanzania tunawachelewesha wengine
kupiga hatua za haraka. Wanadai kama siyo hivyo Jumuiya ya Afrika
Mashariki ingekuwa mbali kwa maendeleo. Maneno hayo yamekuwa yanarudiwa
au kujirudia mara nyingi kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu wa Afrika
Mashariki na hata kwingineko duniani waamini hivyo.
Mheshimiwa Spika;
Napenda kusema kwa dhati ya moyo wangu kwamba madai hayo hayana ukweli
wo wote. Isitoshe hata sababu zinazotolewa kuthibitisha ukweli wake
hazina mashiko. Hazifanani na ukweli kuhusu Tanzania na Watanzania
walivyo. Tanzania ni muumini wa dhati wa umoja na utengamano wa nchi za
Afrika Mashariki na Afrika. Tumethibitisha hivyo kwa vitendo kwa
kuunganisha nchi zetu mbili huru yaani Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na
Jamhuri ya Tanganyika na kuwa taifa moja liitwalo Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Muungano wa nchi zetu mbili ndio pekee uliodumu kwa muda
mrefu kuliko yote Afrika.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni
mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa maana ya
kutekeleza Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo, kwa Itifaki zake na maamuzi
halali ya vikao na taasisi za Jumuiya. Kama lipo jambo ambalo
hatujalifanya ilivyotakiwa itakuwa ni kwa sababu za msingi na siyo kwa
sababu ya kupuuza Jumuiya. Tunaithamini sana Jumuiya na tumeipa
kipaumbele cha juu. Hatuwezi kuhangaika kwa gharama kubwa ya muda wetu,
fedha zetu na kutoa mchango wa hali na mali kuianzisha, kujenga na
kuifikisha Jumuiya hapa ilipo halafu tuwe ni watu tunaoongoza
kutokuipenda na kudhoofisha maendeleo na ustawi wake. Ni maneno ya
kushangaza na wala hayaingii akilini. Ama kweli akutukanae hakuchagulii
tusi.
Mheshimiwa Spika;
Nionavyo mimi msimamo wetu kuhusu
kuharakisha Shirikisho na masuala ya ardhi, ajira, uhamiaji, pengine
ndiyo yanayotuletea hisia zisizokuwa sahihi juu yetu. Mimi siamini kama
kuna mengine. Hata hivyo, napata taabu kuamini kwamba kutofautiana kwa
mawazo katika mambo hayo kutapelekea baadhi ya wenzetu wasipende hata
kushirikiana nasi kwa mambo ambayo hayana matatizo na tumekuwa
tunashirikiana vizuri.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania imekuwa
inawasihi wanachama wenzetu kuwa tujenge Jumuiya yetu hatua moja baada
ya nyingine kama ilivyo kwenye Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Hatuna tatizo la kuongeza kasi ya ujenzi wa Jumuiya lakini
tusivuke hatua yo yote. Tusiende kasi ya kupindukia. Mkataba unaelekeza
tunaanza na Umoja wa Forodha, inafuatia Soko la Pamoja kisha Umoja wa
Kifedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.
Mheshimiwa Spika;
Ni kweli kabisa hatukuunga mkono kuharakisha Shirikisho la Kisasa kabla
ya kukamilisha baadhi ya hatua. Na, tulifanya hivyo kwa nia njema ya
kutaka Shirikisho lijengwe juu ya msingi imara. Na, msingi huo si
mwingine bali utengamano wa kiuchumi kwa maana ya Umoja wa Forodha, Soko
la Pamoja na Umoja wa Kifedha zilizojengeka vizuri na kufanya kazi
ipasavyo na kunufaisha wanachama wote sawia.
Mheshimiwa Spika;
Lazima tutambue ukweli kuwa kunufaika kiuchumi ndicho kichocheo kikubwa
cha nchi kujiunga na kuendelea kuwa mwanachama wa Jumuiya yetu. Kama
mambo ya kiuchumi yakipangika vizuri na kila nchi ikanufaika sawia,
unajenga msingi imara kwa Shirikisho la Kisiasa kustawi na kudumu. Kama
ngazi hizi tatu za awali hazitashughulikiwa vizuri na nchi wanachama
zikahisi hazinufaiki ipasavyo, Shirikisho litayumba au kuyumbishwa hivyo
kudumu kwake kutakuwa kwa mashaka.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni kati ya zile nchi zinazotaka ngazi zote za mchakato wa
utengamano zitekelezwe moja baada ya nyingine bila kuruka hata moja. Kwa
msimamo na mtazamo wetu, Shirikisho iwe ndiyo hatua ya mwisho. Na huo
siyo msimamo wangu au wa Serikali peke yake, ndiyo msimamo wa Watanzania
walio wengi.
Bila ya shaka sote tutakumbuka kuwa mwaka 2006 Wakuu
wa Nchi Wanachama wa Jumuiya waliunda Kamati Maalum katika kila nchi
kukusanya maoni ya wananchi kuhusu kuharakisha Shirikisho la Afrika
Mashariki. Kwa hapa nchini Kamati hiyo iliongozwa na Profesa Samwel
Wangwe na katika taarifa yake, Kamati ilieleza kuwaasilimia 74.4 ya
Watanzania wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho lakini ni asilimia 25.4
tu ndiyo waliunga mkono kuharakishwa kwake.
Mheshimiwa Spika;
Takwimu hizi zinaelezea ukweli kuhusu hisia za Watanzania, kuhusu
kuwepo kwa Shirikisho na kasi ya utekelezaji wake. Watanzania wengi sana
wanaunga mkono kuwepo kwa Shirikisho la Afrika Mashariki lakini
wanataka jambo hilo lisifanywe haraka haraka. Wanataka lifanywe kwa
umakini mkubwa na tuende hatua kwa hatua kama ilivyoainishwa katika
Mkataba uliounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika;
Sera na msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
inakwenda sambamba na ile ya wananchi wa Tanzania. Ndiyo maana tumeafiki
mapendekezo ya Kamati ile ya mwaka 2004iliyoongozwa na Mheshimiwa Amos
Wako wakati ule akiwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya. Kamati hiyo iliundwa
kupendekeza namna ya kuharakisha utekelezaji wa mchakato wa utengamano
wa Afrika Mashariki.
Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umetamka
muda wa kutekeleza ngazi ya Umoja wa Forodha lakini uko kimya kuhusu
ngazi zilizofuata. Ili kuondoa kasoro hiyo na kwa nia ya kuharakisha
Shirikisho Kamati ilipewa jukumu la kutoa maoni na mapendekezo juu ya
namna ya kufanya hivyo. Kamati ilifanya kazi nzuri ya kupata maoni na
hisia za watu wa makundi mbalimbali katika nchi wanachama kuhusu ujenzi
wa Jumuiya na utengamano.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa
Tanzania kwa mfano, Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako ilitambua hisia za
Watanzania kuhusu ardhi na ajira na kupendekezwa kuwa masuala hayo
yabaki kwenye mamlaka ya nchi wanachama kuamua. Kuhusu mchakato wa
utengamano Kamati ilipendekeza kwanza kwamba mchakato wa ujenzi wa Umoja
wa Forodha uachwe mpaka ufike ukomo wake wa miaka mitano. Baada ya hapo
muda wa kutekelezwa ngazi zinazofuata unaweza kupunguzwa. Kwa mfano
walipendekeza kuwa matayarisho ya kuunda Soko la Pamoja yaanze hata
kabla ya mchakato wa Umoja wa Forodha kufika mwisho ili mara wakati huo
ukifikiwa Soko la Pamoja linaanze. Hivyo hivyo mara baada ya ngazi hiyo
kuanza matayarisho ya kuanza ngazi ya Umoja wa Kifedha yanaanza. Ngazi
hiyo nayo ikianza matayarisho ya kuunda Shirikisho yanaanza. Kamati pia
imetoa mapendekezo ya namna ya kufikia uamuzi kuhusu Shirikisho kwamba
wananchi wa nchi wanachama wataamua kwa kura. Tukifuata mapendekezo ya
Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako na wenzake kama tufanyavyo sasa Tanzania
haina matatizo nayo.
Mheshimiwa Spika;
Baada ya kazi kubwa
na nzuri iliyofanywa na wana-Afrika Mashariki kuhusu ujenzi wa Jumuiya
yao inasikitisha kuona vinafanyika vitendo vinavyoanzisha mivutano
kuhusu mambo yaliyokwisha fanyiwa kazi na kuamuliwa. Tunapata taabu
zaidi pale watu wanapobagua wenzao na wanapofanya mambo yanayopingana na
Mkataba wa Jumuiya na Itifaki zake. Kwa kweli kama mwenendo huu
hautabadilika sijui mambo yatakuwaje mbele ya safari.
Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu inapenda kuona kuwa tunakuwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki
iliyo imara na iliyo endelevu. Jumuiya ambayo inaendeshwa vizuri, mambo
yake ni mazuri na nchi zote wanachama na watu wake wananufaika nayo, na
hivyo wanaifurahia. Tanzania haina tatizo na kuharakisha mchakato wa
utengamano, lakini tunapata taabu kuruka baadhi ya hatua kabla
hazijakamilika. Tunawaomba wenzetu kuwa makini katika kila hatua
tunayochukua. Bila ya kufanya hivyo, Jumuiya yetu itakuwa imejengeka
katika msingi dhaifu hivyo ustawi na uhai wake utakuwa na changamoto
nyingi. Hatupendi ya mwaka 1977 yatokee tena.
Mheshimiwa Spika;
Napenda kuwahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushiriki katika
shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuimarisha utengamano wa
Afrika Mashariki kwa kuzingatia matakwa ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki na Itifaki zake. Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa
Jumuiya haidhoofiki wala kufa. Na iwapo itadhoofika au kufa kamwe
hatutaki Tanzania inyooshewe kidole kuwa chanzo wala kichocheo chake.
Ndiyo maana, hatutachoka kuzungumza na wenzetu kuhakikisha kuwa Jumuiya
ya Afrika ya Mashariki inaendelea kustawi.
Tutaendelea kukumbushana
umuhimu wa kufanya mambo yanayojenga na kuepuka yale yanayoweza
kubomoa. Tutakumbushana umuhimu wa kuheshimu matakwa na masharti ya
Mkataba ulioanzisha Jumuiya, Itifaki zake na maamuzi halali ya vikao
rasmi na asasi za Jumuiya. Tukifanya hivyo Jumuiya ya Afrika ya
Mashariki itadumu, itazidi kustawi na kunufaisha nchi wanachama na watu
wake kama yalivyo malengo na madhumuni ya kuundwa kwake.