
Wanajeshi wa Kikosi cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM).
Viongozi
wa Kiafrika wameanza mazungumzo ya kuunda kikosi cha dharura barani
humo kwa ajili ya kuingilia migogoro inayozuka kwa sasa, wakati
wakisubiri mpango wa pamoja wa bara zima kuwa na kikosi maalum cha
jeshi. Mkutano
wa kilele unaohudhuriwa na baadhi ya viongozi wakuu wa bara hilo -
wakiwemo wa Chad, Tanzania na Uganda - mjini Pretoria, Afrika ya Kusini,
ni kuiwezesha Afrika kuingilia kati haraka na ikiwa inajitegemea katika
changamoto za kiusalama zinazolikabili bara hilo, kwa mujibu wa
mwenyeji wa mkutano huo, Rais Jacob Zuma.
"Uamuzi huu
umetokana na kutambua kwamba uingiliaji kati kwenye migogoro yetu
wenyewe hauwezi kusubiri hadi Kikosi Maalum cha Dharura cha bara zima
kiundwe," alisema Zuma.
Hatua za pole pole
Uundwaji wa
kikosi hicho maalum cha Umoja wa Afrika umekuwa ukisuwasuwa tangu
mapendekezo yake ya kuwa na wanajeshi 32,500 na raia kutoka kanda tano
za bara hilo kuanza muongo mzima uliopita.
"Tunaamini
kwamba wakati wa viongozi wa Kiafrika kuweza kuchukua hatua za mpito, za
usalama na za kimaamuzi zinapohitajika umefika," alisema Zuma.
Umoja wa
Afrika ulikosolewa kwa kutochukuwa hatua za haraka dhidi ya mgogoro wa
Mali baada ya jeshi kuchukua madaraka mwezi Machi 2012, na sasa viongozi
hao wanasema wanataka kuhakikisha kwamba hawaonekani wasio uwezo au
walio nyuma sana katika kuchukua hatua bila ya msaada wa mataifa ya nje.
Dhamira mpya
"Afrika
inaweza na ina uwezo na njia za kuchukua hatua. Tunachohitaji ni
kujipanga wenyewe tu," alisema Rais Zuma kwenye mkutano huo.
Inategemewa
kwamba hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu "kutakuwa na mfumo unaoweza
kuhuisha dhamira yetu ya kuwa na umiliki na uongozi wetu wenyewe katika
kukabiliana na changamoto za kiusalama kwenye bara letu tukufu."
Mkutano huo
unahudhuriwa na nchi ambazo zimesema ziko tayari kuchangia kwenye kikosi
hicho, Haikufahamika mara moja ni nchi ngapi kwa sasa ambazo zimeahidi
kutuma wanajeshi wake kuunda kikosi hicho, ambacho kitaitwa "African
Capacity for Immediate Response to Crises (ACIRC)."
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Josephat Charo
Chanzo - DW